STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, November 12, 2011

Miyeyusho aota ubingwa wa dunia



BONDIA machachari, Francis Miyeyusho anayeashikilia taji la UBO-Mabara baada ya kumvua aliyekuwa akilishikilia, Mbwana Matumla, aliyemtwanga hivi karibuni alisema kiu yake kubwa kwa sasa ni kuona anautwaa ubingwa wa dunia katika mchezo huo.
Miyeyusho anayefahamika zaidi kama 'Chichi Mawe', alisema kumvua taji Mbwana ni furaha kubwa, lakini hajaridhika hadi atakapotwaa ubingwa wa dunia katika mchezo huo kama wanavyofanya mabondia wengine duniani.
Bondia huyo, alisema haitakuwa na maana yoyote ya ushindi wake kwa Mbwana kama ataishia kwenye taji hilo la Mabara, ndio maana anasisitiza angependa kuona anafika mbali katika mchezo huo kwa kutwaa ubingwa wa dunia.
"Kiu yangu kubwa kwa sasa ni kuona natwaa ubingwa wa dunia, itakuwa furaha kubwa kuliko hii ya kumvua taji Golden Boy, ambaye ni mmoja kati ya mabondia ninaowaheshimu kwa mafanikio yao nchini kama ilivyo kwa kaka yake," alisema.
Miyeyusho alimtwanga Mbwana kwa pointi katika pambano lao lililofanyika Oktoba 30 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam likiwa ni pambano la tatu kati yao kukutana katika mchezo huo.
Katika mapambano yao ya awali yaliyochezwa Februari 21, 2004 na Januari 17, 2009, Miyeyusho alichezea kichapo toka kwa Mbwana.
Wakati huo huo, bingwa anayeshikilia taji la dunia la World Boxing Forum, Nassib Ramadhan anatarajiwa kupanda ulingoni Desemba 9 kuzipiga na mkenya Anthony Kariuki katika pambano litakalofanyika kwenye ukumbi wa DDC Keko.
Mratibu wa pambano hilo, Pius Aghaton alisema pambano hilo la raundi 10 la uzito wa fly, litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi na lengo kubwa ni kumuandaa Nassib kwa pambano la kutetea taji lake hilo analoshikilia baada ya kumvua aliyekuwa bingwa wake, Juma Fundi, katika pambano lililofanyika nchini Mei mwaka huu.

No comments:

Post a Comment