STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 30, 2012

Simba, Yanga zatishia Super8

USHIRIKI wa Simba na Yanga katika michuano mipya inayotarajiwa kujumuisha timu nane za Tanzania Bara na Visiwaniinayokwenda kwa jina la "BancABC Super 8" uko katika hatikati kutokana na timu hizo kutoiweka ligi hiyo kwenye kalenda zao, imefahamika. Ligi hiyo inayofanana na Ligi ya Muungano inatarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 4 hadi 18 mwaka huu chini ya udhamini wa benki ABC na itajumuisha timu nane. Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema jana kwamba ligi hiyo ni nzuri kwa lengo la kuiandaa timu lakini klabu yake itakuwa radhi kushiriki endapo mgawanyo wa mapato ya mlangoni utabadilishwa na kuwa zaidi ya yale yanayopatikana kwenye mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Rage alisema kwamba klabu zimechoka kunyonywa na hivyo Simba itakuwa tayari kushiriki endapo klabu zitapata mgao wa zaidi ya asilimia 60 ya mapato ya mlangoni. "Ni lazima kwanza tukae na kukubaliana tunapata nini sisi klabu, wakati wa kuona klabu zinanyonywa umepita na sasa kila mkataba ambao TFF watakuwa wameingia wanatakiwa kutushirikisha vilabu ili tujue maslahi yetu," alisema Rage. Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesigwa Selestine aliliambia gazeti hili jana kwamba klabu yake inaona ligi hiyo imeingiliana na programu zao za maandalizi ya msimu ujao wa ligi kuu hivyo maamuzi ya kushiriki au kutoshiriki yatajulikana baada ya kufanyika kwa kikao cha pamoja na benchi la ufundi la timu hiyo. Mwesigwa alisema kwamba mara baada ya kocha mpya, Tom Saintfiet kutua, alipewa ratiba ya michuano iliyopo na hivyo kocha huyo aliandaa programu yake ambayo itaanza kutekelezwa hivi karibuni baada ya mapumziko ya wachezaji kumalizika. "Uwezekano wa timu yetu kushiriki ni mdogo, haikuwa kwenye programu na hivyo inabidi uongozi na benchi la ufundi tujadiliane na kufanya maamuzi yatakayoisaidia timu," alisema katibu huyo. Shirikisho la Soka Nchini (TFF) lilitangaza kusaini mkataba wa miaka mitatu na benki ABC ambayo itadhamini ligi hiyo mpya yenye lengo la kuziandaa klabu kwa ajili ya msimu mpya wa ligi. CHANZO:NIPASHE

No comments:

Post a Comment