ZANZIBAR HEROES USO KWA USO NA AMAVUBI YA NIYONZIMA
Zanzibar Heroes |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
MASHUJAA wa
visiwani, Zanzibar Heroes leo wanatupa kete yao ya pili katika michuano ya
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kwa
kumenyana na Rwanda katika mchezo wa Kundi C, utakaoanza saa 12:00 jioni Uwanja
wa Mandela, Namboole, mjini hapa.
Mchezo huo
utatanguliwa na mchezo mwingine, kati ya Malawi na Eritrea ambao utaanza saa
10:00 jioni kwenye Uwanja huo.
Zanzibar
walilazimishwa sare ya bila kufungana na Eritrea katika mchezo wa kwanza,
wakati Malawi ilifungwa mabao 2-0 na Rwanda.
Zanzibar
wanahitaji kushinda mechi ya leo, ili kuweka hai matumaini ya kuingia Robo
Fainali ya michuano hii, ingawa mbele ya Rwanda huo utakuwa mtihani mgumu kwao.
Moja kati ya
burudani zinazotarajiwa kwenye mechi hiyo ni kushuhudia wachezaji wawili wa
klabu moja, Yanga SC ya Dar es Salaam, beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa
Zanzibar na kiungo Haruna Niyonzima wa Rwanda, wakichuana leo, tena wote wakiwa
manahodha wa timu zao za taifa.
Baada ya
sare katika mechi ya kwanza, Cannavaro pamoja na kuwaomba radhi Wazanzibari kwa
sare hiyo, lakini pia ameahidi watajituma na kufanya vizuri katika mechi
zijazo. CHANZO:BIN ZUBEIRY
No comments:
Post a Comment