Robin va Persie akiifungia bao timu yake ya Manchester United dhidi ya West Ham jana (Picha kwa hisani ya BBC Sports) |
BAO pekee lililoifungwa katika dakika ya kwanza na mshambuliaji nyota wa Kiholanzi, Robin van Persie jana lilizidi kuifanya Manchester United kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England baada ya kuilaza West Ham bao 1-0, huku Liverpool wakilala ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya Tottenham Hotspur.
Ushindi huo wa pili mfululizo kwa Man United ulipataika kwenye dimba lao la Old Trafford na kuwafanya wajikusanyie pointi 33, moja zaidi ya mabingwa watetezi Manchester City waliopata ushindi ugenini wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wao Wigan Athletic.
Mabao ya City, yalifungwa na James Milner katika dakika ya 69 kabla ya Mario Baloteli kuongeza la pili dakika tatu baadae na kuwafanya mabingwa hao kuendeleza rekodi yao ya kuitopoteza mechi yoyote katika ligi hiyo mpaka sasa ikijikusanyia pointi 32 na kushika nafasi ya pili.
Katika pambano jingine lililochezwa kwenye uwanja wa White Hart Line, mjini London, Tottenham iliilaza Liverpool mabao 2-1 na kuzidi kuwafanya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Ulaya kwa timu za Uingereza kuzidi kuyumba kwenye ligi kuu ya England.
Magoli ya Tottenham ya jana yalifungwa na Aaron Lennon dakika ya 7 tu ya mchezo kwa kumalizia kazi nzuri ya kiungo Gareth Bale, ambaye alifunga mwenyewe bao la pili kwa Tottenham dakika ya 16 na kufanya hadi mapumziko wenyeji wawe mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji na kushambuliana kwa zamu Liverpool wakionyesha dhamira ya kurejesha mabao hayo, ambapo Bale katika harakati za kuokoa mabao alijikuta akiifungia wageni bao la kufutia machozi.
Matokeo ya mechi nyingine zilizochezwa jana Southampton ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Norwich City, Stoke City iliilaza Newcastle United mabao 2-1, Swansea City ikaicharaza West Bromwich kwa mabao 3-1 , huku kocha mpya wa Chelsea Rafa Benitez akiendelea kuambulia sare baada ya kikosi chake kutoka suluhu dhidi ya wageni wao Fulham, nao Everton wakiwa nyumbani walilazimishwa sare ya 1-1 na Arsenal.
No comments:
Post a Comment