Zahoro Pazi akiwa katika pozi mbele ya gari lake |
MSHAMBULIAJI wa Azam, Zahoro Pazi, ameweka bayana kwamba hana mpango wa kuzichezea Simba na Yanga kwa sasa kutokana na klabu aliyopo sasa nayo ni miongoni mwa klabu kubwa na zenye malengo ya dhati kisoka.
Pazi, aliyekaribia kutua Simba msimu wa 2010-2011 kwa mkataba wa miaka minne kabla ya 'dili' lake kukwama baada ya Simba kushindwa kutekeleza makubaliano yao na timu ya Mtibwa aliyokuwa anaichezea wakati huo, alisema Azam ni klabu yenye malengo.
Alisema kwa mchezaji yeyote mwenye malengo ya kufika mbali Azam ni klabu sahihi kuichezea, kutokana na kwamba ni klabu inayoioinyesha dhati ya kuleta mabadiliko ya soka nchini na kwa sasa imekuwa miongoni mwa klabu kubwa.
Pazi, ambaye anamaliza mkataba wa kuichezea Azam mwezi ujao, alisema anadhani alifanya maamuzi sahihi kuichezea klabu hiyo, huku akisema hata kama ataachwa katika timu hiyo basi ataelekeza nguvu zake kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
"Sifikirii kuzichezea Simba na Yanga kwa sasa, kama mkataba wangu hautaongezwa Azam basi nitaelekeza nguvu zangu kwenda kucheza soka la kulipwa nje. Japo Simba na Yanga ni klabu kubwa na kongwe, lakini hazina malengo kama Azam," alisema.
Mchezaji huyo ambaye ni mtoto wa kipa nyota wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuwika Simba na Pilsner, Idd Pazi 'Father' alisema kipindi cha nyuma Simba na Yanga zilikuwa kimbilio la wengi kwa sababu hakukuwa na klabu yenye ushindani kama Azam.
Pazi, aliyetua Azam msimu uliopita baada ya kuitumikia Mtibwa Sugar, alisema Simba na Yanga ni timu nzuri na zoefu, lakini kukosekana mipango madhubuti kisoka imezifanya zipige 'maktaimu' kwa muda mrefu licha ya ukongwe wao barani Afrika.
No comments:
Post a Comment