Kocha wa Golden Bush Veterani, Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio' akitoa mawaidha kwa wachezaji wake wakati wa mapumziko ya mechi yao na Wahenga Fc. |
NYOTA wa zamani wa timu za Simba na Yanga, Herry Morris, Shaaban Kisiga 'Marlon' na Athuman Machuppa juzi waliisherehekea vema sikukuu ya Mapinduzi 'mchangani' kwa kuisaidia Golden Bush Veterani kulipa kisasi kwa kuifunga Wahenga Fc mabao 4-3.
Wachezaji hao watatu waliifungia timu hiyo ya Golden Bush iliyokuwa imesheheni nyota wa zamani wa klabu hizo kongwe na Mtibwa Sugar, bao moja moja na kuisaidia kulipa kisasi cha kipigo cha idadi kama hiyo waliyopewa wakati wakiuaga mwaka 2012.
Nyota hao wakishirikiana na akina Wazir Mahadhi 'Mandieta', Shija Katina, Said Swedi 'Panucci', Salum Swedi 'Kussi' na Wisdom Ndlhovu waking'ara katika mchezo huo uliofanyika kwenye uwanja wa TP-Sinza kusherehekea Mapinduzi na kuukaribisha 2013.
Morris, alianza kuifungia timu hiyo mabao mawili katika dakika ya sita kwa shuti kali kabla ya kuongeza jingine dakika ya 31 kwa kumpiga chenga kipa wa Wahenga, Davi 'Seaman' aliyetoka langoni mwake kumkabili.
Hata hivyo dakika mbili baadae Wahenga walipata bao lao la kwanza kupitia God 'Wanchope' kabla ya beki wao wa kulia, Shomar Pengo kufunga bao la pili na la kusawazisha la Wahenga na kufanya hadi mapumziki matokeo yawe mabao 2-2.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu kufanya mabadiliko na Golden Bush iliongeza bao la tatu kupitia Kisiga aliyefunga kwa mkwaju wa penati baada ya beki mmoja wa Wahenga kuunawa mpira langoni mwake.
Athuman Machuppa aliihakikishia Golden Bush baada ya kuifungia bao la nne katika dakika ya 81 kwa kuunganisha pasi murua ya Morris aliyekuwa nyota wa mchezo huo.
Dakika moja kabla ya pambano hilo Wahenga walipata bao la tatu kwa mkwaju wa penati uliotumbukizwa wavuni na kiungo wao nyota, Macocha Mayay baada ya mabeki wa Golden Bush kucheza madhambi langoni mwao.
No comments:
Post a Comment