Rooney akipachika mpira wavuni |
MABAO mawili yaliyopachikwa wavuni na mshambuliaji Wayne Rooney imeiwezesha Manchester United kuendelea kujikita kileleni mwea msimamo wa Ligi Kuu ya England baada ya kuilaza Southampton kwa mabao 2-1 katika mfululizo wa ligi hiyo.
Mashetani hao Wekundu waliokuwa uwanja wao wa nyumbani wa Old Trafoord, walijikuta wakishtukizwa kwa kufungwa bao la mapema na wageni wao lililofungwa na Jay Rodriguez dakika ya tatu tu ya mchezo huo, hata hivyo dakika tano baadae Rooney aliwatuliza mashabiki wa timu yake kwa kusawazisha bao.
Rooney aliendelea kung'ara kwa kuongeza bao la pili dakika ya 27 akimalizia kazi nzuri ya Patric Evra na kufanya hadi mapumziko timu hizo ziwe zimefungana mabao 2-1 yaliyomudu hadi zilipomalizika dakika 90 za pambano hilo.
Kwa ushindi huo Manchester imeongeza pengo la pointi saba kati yao na wapinzani wao, Manchester City ambayo juzi ililazimishwa sare na kusalia na pointi zao 52 huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 24 kila mmoja.
Katika mapambano mengine yaliyochezwa usiku wa jana, Liverpool iliwabana wenyeji wao Arsenal na kufungana nao mabao 2-2, huku Norwich City ilijikuta ikibanwa mbavu nyumbani kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1.
Nayo Reading iliing'ang'ania waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Chelsea kwa kufungana nao magoli 2-2 na Fulham iliicharaza West Ham United mabao 3-1 na Everton iliendeleza maajabu wake msimu huu kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 mbele ya West Bromwich.
Ligi hiyo inatarajiwa kuingia mzunguko wa 25 mwishoni mwa wiki kwa mechi katika viwanja mbalimbali nchini humo.
Rooney akishangilia moja ya mabao yake ya jana |
No comments:
Post a Comment