Kocha wa Mtibwa Mecky Mexime |
TIMU ya soka ya Mtibwa Sugar imesema imejiandaa vya kutosha kuweza kuwakabili vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga watakaovaana nao keshokutwa jijini Dar es Salaam.
Mtibwa inatarajiwa kuvaana na Yanga katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo duru la pili ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 walichopewa nyumbani kwao na Polisi Morogoro.
Katika pambano lao la awali Mtibwa iliisasambua Yanga mjini Morogoro kwa mabao 3-0, hali inayofanya pambano hilo la marudiano kuwa la aina yake, ndio maana benchi la ufundi la timu hiyo limedai kuwa limepania kurekebisha makosa mbele ya wapinzani wao wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa sasa.
Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime, amesema kuwa kikosi chao kipo katika hali nzuri kuweza kuikabili Yanga na kuendeleza ubabe wao, licha ya kukiri wanatarajia upinzani mkali.
Mexime, alisema hana shaka na pambano hilo kwa namna alivyoweza kurekebisha makosa yaliyowagharimu katika pambano lao lililopita walilopoteza nyumbani.
"Tumejiandaa na tupo tayari kuivaa Yanga na hatuna hofu yoyote, vijana wangu wapo kamili kuweza kurekebisha makosa yaliyotuponza kwa Polisi Moro," alisema Mexime.
Mexime, alisema ushindi pekee ndiyo kitu kinachohitajika kwa Mtibwa ili kuweza kujipanga kwa ajili ya kumaliza nafasi za juu mwishoni mwa msimu.
Mbali na mechi hiyo ya Yanga na Mtibwa, siku hiyo ya jumamosi kutakuwa na mechi nyingine kadhaa kabla ya Jumapili Mabingwa watetezi, Simba kuvaana na JKT Ruvu ambayo .inatarajiwa kumtumia nyota wqa zamani za Msimbani Mussa Hassani Mgosi kuweza kuwasimamisha Simba walioilaza Africans Lyon katika mechi yao iliyopita.
No comments:
Post a Comment