BONDIA Albinus Felesianu wa Namibia leo
ameudhihirishia ulimwengu kuwa yeye kweli ndiye Mfalme wa uzito wa unyoya
duniani kwa vijana baada ya kumgalagaza bondia Herbert Quartey wa Ghana katika
mpambano wao uliofanyika katika ukumbi wa Windhoek Country Club Resort and
Casino leo tarehe 29, March 2013.
Umati wa watu wasiopungua elfu 20 walijazana katika ukumbi huo wa
burudani wakimshangilia kwa nderemo na vifijo bondia wao Albinus wakati
alipokuwa anafanya vitu vyake kwenye ulingo.
Baada ya mtangazaji wa ulingo kutamka kuwa “Na sasa bingwa mpya
wa uzito wa unyoya duniani kwa vijana ni Albinus Felesianu” mayowe ya
wapenzi wa ngumi waliojazana katika ukumbi huo yaliweza kusikika kilometa tatu
mpaka katikati ya jiji la Windhoek.
Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa Albinus kuunyakua mkanda wa
ubingwa wa dunia kwa vijana kwani Mghana Herbert Quartey naye alikuwa mbogo
kwani alirusha kila aina ya masumbwi yaliyomo kwenye kitabu.
Wawili hao walichapana makonde mazito kama watu wenye uzito mkubwa
na kama sio uwezo na ujuzi wa referii Deon Dwarte wa Afrika ya Kusini kazi
ingekuwa ngumu sana kwani kila bondia alijaribu kumpata mwenzake katika sehemu
zinazoumiza ili kuumaliza mpambano mapema lakini ujuzi na ubishi wa kila mmoja
ulifanya kusiweko na knockout yoyote!
Hii ni mara ya kwanza kwa nchi ya Namibia kuweza kuandaa mpambano
wa ubingwa wa dunia wa IBF na wakali hao waliweza kuufanya umati wote
uliohudhuria kulipuka kwa makelele ya kushangilia kila wakati.
Alikuweko Harry Simon, ambaye ndiye Mnamibia aliyeweza kuufanya mchezo
wa ngumi kupendwa na kuwa maarufu sana nchini humu. Uwezo na utukutu wa Harry
Simon ulingoni umeufanya mchezo wa ngumi kupendwa karibu na kila Mnamibia.
Walikuweko pia wageni wengine wengi lakini kampuni ya simu ya
Telecom ambayo ndio waliokuwa wadhamini wa mpambano huo imejikusanya kila aina
ya sifa na upendo kutoka kwa wananchi wa Namibia jinsi inavyo dhamini mchezo wa
ngumi!
Mpambano huu uliandaliwa na Kinda Nangolo wa kampuni ya Kinda
Boxing Promotions ambayo ndio waandaaji wa mpambano ujao wa mwezi wa Mei wa
bingwa wa IBF Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati katika uzito wa
unyoya bondia Gottlieb Ndokosho. Mpambano wa IBF wa Kimataifa wa bondia Harry
Simon nao utafanyika mwezi wa Juni.
Aidha, Immanuel “Prince’ Naidjala”wa Namibia na Lesley Sekotswe wa
Botswana watarudiana tena mwezi wa July kumpata bingwa wa kimataifa wa uzito wa
bantam baada ya kutoka sare walipokitana wiki iliyopota nchini Namibia.
No comments:
Post a Comment