STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 30, 2013

Simba kutema ubingwa leo? Azam, Ruvu patachimbika Pwani


Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba

Azam watakaovaana na Ruvu Shooting mkoani Pwani
USHINDI wowote itakayopata  vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga  kwenye pambano lake dhidi ya Polisi Moro jioni ya leo na watani zao Simba kueteleza jijini Mwanza mbele ya Toto African itaipa Yanga nafasi ya kulishika taji la ubingwa kwa mkono mmoja ikisubiri kukabidhiwa rasmi mechi mbili zijazo.

Yanga itashuka dimba la Jamhuri kumenyana na wenyeji wao, ikiwa ina pointi 48 kibindoni, huku watani zao wanaoshikilia taji hilo kwa sasa wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 34, sita nyuma ya wanaoshika nafasi ya pili Azam itakayokuwa dimba la Mabatini-Mlandizi, Pwani kuumana na wenyeji wao Ruvu Shooting.

Simba inahitajika kupata ushindi katika mechi yake ya leo itakayopigwa CCM Kirumba iwapo inahitaji kuendelea kutambulika kama bingwa mtetezi, kwani matokeo yoyote kinyume na ushindi itakuwa imelipema rasmi taji hilo na kuliachwa likigombewa na timu za Yanga na Azam.

Tayari kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu na baadhi ya wachezaji wa kikosi cha mabingwa hao wameapa kufa kiume leo Kirumba ili kufuta machungu ya kugaragazwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mechi yao iliyopita iliyochezwa siku ya Jumatano.

Julio alisema licha ya kuwakosa wachezaji wake kadhaa wakiwemo 'mapro', Mussa Mudde na Abel Dhaira na kuumia kwa Kiggy Makassy na Haruna Chanongo kuwa na hatihati ya kucheza leo, bado anaamini kikosi chake kitafanya vyema mbele ya Toto.

Hata hivyo kocha wa Toto, Athuman Bilal 'Bilo' alinukuliwa jana akisema kuwa wanaichukulia mechi yao ya leo kama fainali kwa kuhitaji pointi tatu muhimu ili wajinasue eneo la mkiani linalotishia kuirudisha timu yake kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Mechi nyingine za leo Azam watakuwa wakiendeleza harakati zao za kuifukizia Yanga kileleni kwa kuumana na Ruvu Shooting inayonolewa na kocha Charles Boniface Mkwasa.
Azam inahitaji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kuweka rekodi ya kuwa bingwa wa Tanzania iwapo Yanga itateleza kileleni, licha ya kwamba imeachwa nyuma pointi 8 mpaka sasa.
Azam inaivaa Ruvu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 iliyopata kwa Prisons Mbeya, na ikiwa inajiandaa kurudiana na Barracks YCII ya Liberia katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mtibwa Sugar imesafiri mpaka Kagera kwa ndugu zao Kagera Sugar wanaoendelea kuchekelea ushindi dhidi ya Simba juzi Jumatano, kila moja ikisaka ushindi na pointi tatu kuimarisha nafasi yake katika msimamo wa Ligi hiyo inayoelekea ukingoni kwa sasa.
JKT Ruvu waliozinduka katrika mechi yao ya mwisho kwa kuilaza Polisi Moro mabao 3-2 itakuwa ugenini uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta, jijini Arusha kuumana na wenyeji wao JKT Oljoro iliyo chini ya kocha Mbwana Makatta.
Pambano la mwisho kwa mujibu wa ratiba inayoonyesha kuwa Coastal Union wamesafiri kutoka Tanga kuja Dar kuumana na African Lyon katika pambano linalotarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Chamazi, huku Mgambo Shooting watakuwa wakila shushushu kama ilivyo kwa Prisons ya Mbeya.
Je ni timu ipi italia au kucheza jioni ya leo? Bila shaka ni jambo la kusubiri kuona baada ya dakika za 90 za mapambano hayo.

No comments:

Post a Comment