Garreth Bale akifunga bao la kwanza la Tottenham jana dhidi ya Inter Milan |
TIMU ya soka ya Tottenham Hotspurs ya Uingereza jana iliendelea kufanya vema katika harakati zake za kuwania ubingwa wa Ligi Ndogo ya Ulaya baada ya kuinyuka Inter Milan ya Italia mabao 3-0 wakati 'ndugu' zao wa London, Chelsea wakinyukwa bao 1-0 na Steaua Bucurest katika michuano hiyo.
Mabao mawili ya kipindi cha kwanza kupitia kwa winga mahiri, Garreth Bale katika dakika ya sita na lile la Gylfi Sigurdsson la dakika ya 18 na la kipindi cha pili kupitia beki wao, Jan Verlonghen yalitosha kuipa nafasi kubwa ya Tottenham kunusa robo fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu.
Katika mechi nyingine zilizochezwa usiku wa jana katika mechi hizo kuwania kutinga robo fainali, Chelsea walidunguliwa bao 1-0 ugenini na Steaua Bucurest, huku Newcastle United ililazimisha suluhu ugenini dhidi ya matajiri wa Urussi, Anzhi Makhachkala.
Viktoria Plzeň ilikubali kipigo nyumbani kwao kwa kulazwa bao 1-0 na Fenerbahçe, Lazio ya Italia ikapata ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Stuttgart ya Ujerumani,huku Levante ikiwa nyumbani Hispania ililazimishwa suluhu na Rubin Kazan.
Mechi nyingine ilishuhudiwa Basel ikiinyuka Zenith mabao 2-0, na Benfica ikiwa nyumbani Ureno iliinyuka Bordeaux ya Ufaransa bao 1-0. Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki ijayo kujua zipi zitakazopenya robo fainali.
No comments:
Post a Comment