STRIKA
USILIKOSE
Tuesday, April 23, 2013
Vita ya Dunia Bayern na Barca Ligi ya Mabingwas Ulaya
MUNICH, Ujerumani
KOCHA Pep Guardiola siyo peke yake anayechukuliwa kuwa ni kiunganishi kati ya Bayern Munich na Barcelona, ambazo zinakutana leo katika mechi yao ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Allianz Arena nchini Ujerumani.
Timu zote mbili zinatawala katika ligi kuu zao, zimetwaa mataji ya Ulaya mara nne kila moja, zina ushindani mkali dhidi ya Real Madrid, na pia zote zimewahi kufundishwa na kocha mwenye majivuno, Mholanzi Louis van Gaal.
Zote pia zimewahi kufika fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara mbili katika miaka minne iliyopita, ingawa Barca walitwaa ubingwa katika fainali hizo na Bayern wakiambulia patupu.
Barcelona wako kileleni mwa msimamo wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwa tofauti ya pointi 13, lakini bado wanapewa nafasi ndogo ya kushinda dhidi ya 'wauaji' Bayern, ambao walishatwaa taji la Bundesliga, Ligi Kuu ya Ujerumani wiki mbili zilizopita na kupata ushindi mnono wa mabao 6-1 katika kila mchezo miongoni mwa mechi mbili zilizofuatia, tena wakitumia wachezaji wao wengi wa akiba.
"Wachezaji wanafurahia soka lao, na tuko katika hali nzuri sana. Kila mmoja amehamasika, tunacheza soka lenye pasi za kuvutia, tunaonyesha nidhamu ya hali ya juu, na tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga magoli," alisema kocha Jupp Heynckes baada ya ushindi wao wa 6-1 dhidi ya Hanover 96 Jumamosi.
"Kwa mara nyingine tena, wachezaji wameonyesha kwamba hatuna timu ya kikosi B, tuna kikosi A tupu."
Ubabe wa Barcelona katika La Liga umeibua madai kutoka kwenye vyombo vya habari vya Madrid kwamba sasa imekuwa ni kawaida yao na kwamba hawatashangilia kwa kutwaa ubingwa msimu huu.
"Inaelekea kuna watu wanataka kuonyesha kwamba ubingwa wa ligi kuu ya Hispania si lolote, lakini hilo si la kweli, ni taji muhimu sana," alisema kiungo wa Barca, Cesc Fabregas.
Bayern wanaamini kwamba uchezaji wao na sera zao katika kuinua vipaji vya wazawa vinawafanya walingane kwa kila hali na Barcelona na hicho ndicho kilichowafanya wamtwae Guardiola, ambaye aliondoka Barca mwisho wa msimu uliopita ili aanze kuwaongoza kuanzia msimu ujao.
Rais wa Bayern, Uli Hoeness, alifichua hivi karibuni kwamba Bayern walianza mazungumzo na Guardiola kwa muda mrefu kabla hajawakubalia Januari.
"Nilihisi kitambo kwamba Bayern ni klabu ambayo inafanana sana katika masuala ya soka na Barcelona, kwahiyo haikuwa kazi kubwa kumshawishi," alisema Hoeness.
Cha kushangaza, hadi sasa kumekuwa na mechi sita tu zilizowahi kuwakutanisha Barcelona na Bayern, ambao watawakosa nyota wao Mario Mandzukic anayetumikia adhabu na majeruhi Toni Kroos.
Katika mechi yao ya mwisho iliyokuwa ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya miaka minne iliyopita, ilichezwa wakati Bayern ikiongozwa na kocha Juergen Klinsmann na katika mechi yao ya kwanza, Barca ilishinda
4-0 kwa mabao ya kipindi cha kwanza na katika marudiano, walifungana 1-1.
"Naikumbuka sana mechi ile na sitaki kuifikiria kwa sababu ilikuwa ikituumiza sana kuitazama," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge.
"Hata hivyo, sasa ni fursa nzuri kwetu kuonyesha kuwa tumeimarika."
Barcelona watawakosa majeruhi Javier Mascherano na Carles Puyol, hivyo kumuacha kocha Jordi Roura akiumiza kichwa ampange mchezaji gani wa kuanza kikosini na Gerard Pique katika nafasi ya ulinzi wa kati.
Vikosi vinavyotarajiwa leo:
Bayern Munich: Manuel Neuer; Philipp Lahm, Daniel van Buyten, Dante, David Alaba; Bastian Schweinsteiger, Javi Martinez; Thomas Mueller, Franck Ribery, Arjen Robben na Mario Gomez
Barcelona: Victor Valdes; Daniel Alves, Gerard Pique, Eric Abidal, Jordi Alba; Xavi, Sergio Busquets, Andres Iniesta; Alexis Sanchez, Lionel Messi na Pedro .
------
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment