Kikosi cha Simba |
Mabingwa Yanga wakiwa na taji lao la Kagame |
JOTO la mechi ya wapinzani jadi baina ya Yanga na Simba lilizidi kupanda jana kwa miamba hao wa soka nchini kujikuta wakilumbana kwa kitu ambacho shirikisho la soka nchini (TFF) limesema ni uzushi mtupu.
Viongozi wa Simba, Yanga walihusika katika mijadala mizito huku mashabiki wakitoa maoni mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kufuatia taarifa kwamba refa wa mechi hiyo alipaswa kuwa ni Israel Nkongo lakini TFF imembadilisha na kumweka Martin Saanya.
Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kwamba shirikisho hilo halikuwahi kumtangaza mwamuzi wa mechi hiyo kabla ya kumtangaza Saanya.
"Hizo habari kwamba mwamuzi amebadilishwa zimetoka wapi? Tulikuwa hatujamtangaza refa wa mechi na tulipotangaza tumemtangaza Saanya kwa hiyo hamna refa aliyebadilishwa," alisema.
Uvumi wa kubadilishwa refa ulizua kauli mbalimbali za viongozi huku kiongozi mmoja wa Simba akidaiwa kusema kwamba hawataingiza timu uwanjani, jambo ambalo kwa mujibu wa kanuni litawashuhudia wakishushwa daraja.
Kanuni za ligi, hata hivyo, zinaruhusu mwamuzi kubadilishwa hadi saa nane kabla ya mechi.
Akizungumza jana Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema "Simba itacheza dhidi ya Yanga hata kama TFF itabadili uwanja na kuipeleka kwenye Uwanja wa Kaunda" unaomilikiwa na Yanga, huku akisisitiza kwamba kubadili mwamuzi kunaipaka matope TFF kwani jambo hilo halipo katika nchi nyingine.
Katibu Mkuu wa Lawrance Mwalusako alisema kuwa wao hawajali ni mwamuzi gani amepangwa kuchezesha mechi hiyo.
"Sisi hatuna tatizo katika hilo, TFF ndiyo wenye jukumu la kuamua mwamuzi gani achezeshe, Simba kulalamika ni dalili za mchecheto dhidi yetu," alisema.
Mwalusako alisema tishio la Simba ni dalili za wazi za kuanza mapema kutafuta visingizio baada ya kubaini kuwa kikosi chao hakina ubavu wa kuwahimili vijana wa Jangwani.
Bungeni Dodoma nako wabunge waliendeleza kuizungumzia mechi hiyo.
Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Mahmoud Mgimwa (CCM), alisema ubingwa wa Yanga hautanoga iwapo timu hiyo haitaifunga Simba katika mechi ya marudiano keshokutwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
“Naipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa lakini nawaagiza viongozi wake kuwa bila kuifunga Simba ubingwa huo hautanoga,” alisema.
Mgimwa aliyasema hayo bungeni jana mara baada ya kusoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara kuhusiana na hotuba ya bajeti ya Viwanda na Bishara kwa mwaka 2013/2014.
Alisema kwa kuifunga Simba, kutaboresha safari ya mtani wao ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Aden Rage (Mbunge wa Tabora Mjini-CCM).
Awali, mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha asubuhi cha maswali na majibu kilichokuwa kinaongozwa na Mwenyekiti wa kamati ya Bunge, Mussa Zungu, aliipongeza Yanga kwa kuchukua ubingwa.
“Na humu ndani tupo wengi sana na nina fanya hivyo kwa kuwa mimi ni Mbunge wa Ilala ambaye Yanga ipo jimboni kwangu,” alisema.
Tangu Jumatatu wiki hii, kumekuwa na matambo kati ya wabunge wanaoziunga mkono timu hizo ndani ya Bunge mara wanapopata nafasi.
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani, (CCM), ambaye ni shabiki wa Simba, alikaririwa na gazeti hili akiwataka wabunge wenzie kwenda katika eneo wanalofanyia vikao vyao la Msalato (nje kidogo ya Mji wa Dodoma), kupanga mikakati ya ushindi dhidi ya Yanga.
Simba iko Unguja na Yanga iko Pemba katika kambi za kujiandaa na mechi hiyo ya kukamilisha ratiba baada ya Yanga kuwa imeshatwaa ubingwa huku Simba ikiwa haiwezi kufuzu kucheza michuano ya Afrika.
No comments:
Post a Comment