STRIKA
USILIKOSE
Friday, May 17, 2013
Kivumbi cha RCL kwa mechi za marudiano kutimka wikiendi
Na Boniface Wambura
Mechi za marudiano za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zinachezwa wikiendi hii katika viwanja kumi tofauti wakati mechi ya Flamingo ya Arusha na Machava FC ya Kilimanjaro yenyewe itachezwa Jumatatu (Mei 20 mwaka huu).
Uamuzi wa mechi hiyo kuchezwa Jumatatu ni kutokana na Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid kutumika kwa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kesho wakati Jumapili utatumika kwa shughuli nyingine za kijamii kwa mujibu wa wamiliki wa uwanja huo (CCM Mkoa wa Arusha).
Mechi nyingine zitachezwa keshokutwa (Jumapili) ambapo Abajalo watakuwa wenyeji wa Red Coast kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara utatumika kwa mechi kati ya wenyeji Coast United na Kariakoo ya Lindi.
African Sports ya Tanga itaoneshana kazi na Techfort ya Ifakara mkoani Morogoro katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkwakwani. Nayo Simiyu United ya Simiyu itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa Namfua, mjini Singida.
Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ndiyo utakaotumika kuzikutanisha timu za Polisi Jamii Bunda kutoka Mara na wenyeji UDC wakati Biharamulo FC ya Kagera na Polisi SC ya Geita zitaumana kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Milambo FC ya Tabora itakuwa mwenyeji wa Saigon FC ya Kigoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora huku Mbinga United ya Ruvuma ikiikaribisha Njombe Mji ya Njombe kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa utatumika kwa mechi kati ya wenyeji 841 KJ dhidi ya Kimondo SC kutoka Mbeya. Nazo Rukwa United na Katavi Warriors zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.
Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya pili zitacheza mechi zao za kwanza kati ya Mei 25 na 26 mwaka huu wakati mechi za marudiano ni kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment