STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, July 23, 2013

Huyu ndiye Hussein Javu mkali wa mabao wa Mtibwa Sugar

Javu wa tatu toka kushoto akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar
Jamaa nouma, Ona alivyuowaacha akina Himid katika pambano baina ya timu zao
Hapa akijifua katika timu ya taifa, Taifa Stars
moza
Akiwajibika uwanjani na kikosi cha Stars
Akitokelezea kibrazamen akiwa home
INGAWA anadai amefunga magoli mengi kiasi hakumbuki idadi yake kamili, lakini Husseni Javu anasema mabao aliyowafunga Yanga katika pambano la duru la kwanza la Ligi Kuu msimu uliopita ndiyo matamu asiyoyasahau kwa urahisi.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Sept. 19, mwaka jana, mshambuliaji huyo nyota wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, alifunga magoli mawili yaliyotosha kuipa Mtibwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Yanga na kusababisha aliyekuwa kocha wa timu hiyo ya Jangwani, Tom Saintfied kutimuliwa klabuni hapo akiwa na siku 77 tu.
Javu anasema kwa jinsi alivyoyafunga kiufundi na kuzima ngebe za wapinzani wao waliotamba kushinda kabla ya pambano hilo ndiyo inayomfanya asiyasahau.
"Kwa yeyote aliyeyaona atakubaliana nami yalikuwa ya ufundi na kubwa zaidi ni kukata kilimilimi cha Yanga kwa kuwalaza mabao 3-0 licha ya tambo zao kwamba wangetuchapa Jamhuri," anasema.
Javu shabiki mkubwa wa Manchester United na anayemhofia beki wa zamani wa Simba aliyetua Coastal Union, Juma Nyosso anasema hata hivyo pambano gumu kwake lisilofutika kichwani ni lile la Mtibwa na Mgambo JKT.
Anasema anaikumbuka mechi hiyo ya duru la pili lililochezwa Mkwakwani Tanga kwa sababu ya kuchezewa vibaya na beki aliyekabana naye asiyemkumbuka jina kiasi cha kumtia hasira na kulimwa kadi ya njano kabla ya kocha wake Mecky Mexime kumpumzisha ili kumwepusha na kadi nyekundu.
"Sijawahi kukutana na mechi ngumu kama ile ya Mgambo JKT hasa beki yake iliyokuwa inacheza kwa vurugu hadi nikapewa kadi ya njano na kumfanya kocha anitoe nje,"anasema.
Anasema licha ya vurugu hizo anashukuru Mtibwa walishinda bao 1-0 kupitia Salvatory Mtebe.

YANGA
Javu aliyeanza soka tangu akisoma Shule ya Msingi Turiani-Kilimanjaro, Morogoro na chandimu akikipiga Mwembeni Stars, amekuwa akitajwa kutua Yanga kwa msimu ujao, japo mwenyewe ameziruka taarifa hizo.
Mkali huyo ambaye hajaoa japo ana mchumba na watoto wawili kati ya watatu aliyokuwa nao baada ya mmoja kufariki, anakiri Yanga na Simba zilishamfuata kumtaka ajiunge nazo, ila hajasaini kokote.
"Sijasaini kokote kwani Simba na Yanga ziliponifuata nilizieleza nina mkataba na Mtibwa hivyo wazungumze na viongozi ili waafikiane," anasema.
Anadai tangu baada ya hapo hajajulishwa chochote na kushangaa kudaiwa  ameshamwaga wino Jangwani, huku akizushiwa pia ni majeruhi wa kudumu.
"Taarifa hizi zinashangaza wakati ni juzi tu tumemaliza ligi na kuichezea Mtibwa karibu mechi zote sasa majeraha hayo yametoka wapi," anahoji.
Anadai taarifa hizo zimempa usumbufu kwa kocha na daktari wake wakidhani aliumia kwenye 'ndondo' wakati hazina ukweli.
Javu anayependa kula chakula kizuri kwa afya na kunywa juisi , anasema kama Yanga na Mtibwa wamekubaliana juu yake, yeye hajajulishwa.
Hata hivyo anasema kama Yanga imemtaka kweli wamalizane na uongozi wake anaodai anauheshimu kwa kumtoa mbali kisoka tangu alipotua timu ya vijana enzi za kocha anayemsifia 'King' Abdallah Kibadeni.
"Hakuna asiyependa kuzichezea timu kubwa hivyo Yanga wakimalizana na Mtibwa nami nikaridhishwa na masilahi sitakuwa na tatizo lolote, soka ni ajira yangu na kokote nacheza,"anasema.
Javu (kulia) akiwa na jamaa yake Bakar Seblungo 'Beka'

TUZO
Hussein Omar Javu, alizaliwa Februari 16, 1988 Turiani Morogoro akiwa mtoto wa pili kati ya sita wa familia yao na alisoma Shule ya Msingi Turiani Kilimanjaro kabla ya kubobea jumla katika soka.
Anasema wakati akiibuka katika soka alikuwa akiitwa Hussein Masha, bila kujua sababu, ingawa anamkumbuka nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba na Pamba, Simba na Taifa Stars.
"Mtaani walikuwa wakiniita Masha, cha ajabu Masha alikuwa kiungo mimi tangu utoto nacheza ushambuliaji ila nililizoea jina hilo,"anasema. 
Anasema wakati akiichezea chandimu aliumia tumboni na kumfanya baba yake amzuie kucheza kwa miaka mitatu kabla ya kubembelezwa wadau wa soka kijijini kwao wakiongozwa na Mzee Hamis Cheza na kurejea tena uwanjani.
"Kama siyo Mzee Hamis sidhani kama ningecheza tena kwani baba hakutaka kusikia habari za soka akihofia ningeumia tena, niliporuhusiwa nilijiunga Kingstone." anasema.
Mkali huyo anayeitaka serikali kuwekeza katika soka la vijana kwa kuboresha shule za michezo hasa kuzisaidia 'academia' zilizopo ili kuibua na kukuza vipaji, anasema baada ya kuichezea Kingstone katika Ligi Daraja la Tatu alihamia kwa mahasimu wao Docks na kuongeza uhamasa mkubwa mpaka sasa.
Alipokuwa Docks alifuatwa na Alphonce Modest kumshawishi ajiunge Mtibwa iliyokuwa ikisaka vijana wa kuunda timu ya vijana ambapo hata hivyo alikataliwa kabla ya Kibadeni kumkingia kifua na kumbakisha akishajiliwa mwaka 2007.
Akiwa na timu ya vijana walishiriki michuano ya Uhai na kufanikiwa kuibuka  Mfungaji Bora akiifungia timu yake iliyomaliza nafasi ya tatu jumla ya mabao 7.
Javu anasema kabla ya tuzo hiyo alishanyakua tuzo nyingine kama hiyo katika michuano kadhaa ya mchangani mjini Morogoro na ameendeleza moto wa mabao hata alipopandishwa timu ya wakubwa ya Mtibwa aliyonayo mpaka sasa.
Anasema japo hajapata mafanikio makubwa katika soka, anashukuru amenunua kiwanja, kutwaa tuzo na mataji kadhaa kama ya Tusker na Mapinduzi akiwa na Mtibwa mbali na kumudu maisha na familia yake.
Ndoto za Javu ni kucheza soka la kulipwa na anasema analizwa na kifo cha mwanae huku akiwataja King Kibadeni, wazazi wake, rafikie Bakari Seblungo na kaka yake Mrisho Javu kama waliomsaidia kufika alipo.
Javu anayewataka wachezaji wenzake kupendana na kuzingatia nidhamu anadai anaimani kubwa Stars kufuzu fainali za CHAN kwa mara ya pili baada ya zile za mwaka 2009.

No comments:

Post a Comment