Kim Poulsen |
Na Boniface Wambura
KOCHA
Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kikosi chake kimejiandaa
kuikabili Uganda kwenye mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi ya
kucheza Fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN)
itakayochezwa Jumamosi jijini Kampala.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Mwanza leo, Kim amesema tangu kikosi
chake kimeingia kambini Julai 14 mwaka huu, wachezaji wamekuwa wakifanya
vizuri kwenye mazoezi na wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo.
“Uganda
ni timu bora kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Mechi itakuwa
ngumu, tunaamini tunakwenda kufanya vizuri. Tayari tunayo mikakati kwa
ajili ya mechi hiyo, tunakwenda kuikamilisha Kampala,” amesema Kim.
“Hiki
ni kipindi kigumu kwa mpira wa miguu, na suala la kufunga ni la kiimani
ambapo hatuwezi kuwazuia wachezaji kufunga. Karibu nusu ya wachezaji
wanafunga, hii ni changamoto ambayo tunaiheshimu,” amesema Kim na
kuongeza kuwa ni wazi kikosi chake cha kwanza kitakuwa na mabadiliko
baada ya beki Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio nchini Uholanzi.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaondoka Mwanza
kesho (Julai 24 mwaka huu) saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir na
kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 8.15 mchana.
Wachezaji
waliomo kwenye msafara huo ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali
Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin
Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
Viungo
ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis
Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni
John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
No comments:
Post a Comment