STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, August 17, 2013

Askari Kanzu anaswa Msikiti wa Mtambani 'atekwa' kwa muda na waumini



Baadhi ya waumini wa Kiislamu Msikiti wa Mtambani wakiwa wamemzunguka askari Polisi, Jonathan Tossi (katikati aliyeshika kamera) wakimuhoji baada ya kumshikilia kwa muda, hata hivyo walimuachia kwa masharti ya kumtaka afute picha zote alizopiga eneo hilo.

Askari Polisi wakizunguka doria eneo la Msikiti wa Mtambani jijini Dar es Salaam kuhakikisha kuna amani.

Askari wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakizunguka kufanya doria maeneo mbalimbali ya jijini la Dar es Salaam kuhakikisha kuna amani. (Picha kwa hisani ya Gazeti la Jambo Leo.)
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BAADHI ya waumini wa Kiislamu Msikiti wa Mtambani Jijini Dar es Salaam jana wamemkamata mmoja wa askari wa Jeshi la Polisi na kumshikilia kwa muda kabla ya kumwachia kwa masharti kadhaa. 
Kwa mujibu wa chanzo cha habari hizi kimebainisha askari aliyekamatwa ni Jonathan Tossi ambaye anafanya kazi kitengo cha habari na uhusiano wa Jeshi la Polisi.

Askari huyo alijikuta akiingia kwenye mikono ya waumini hao alipokuwa akitekeleza majukumu yake (kazini) akipiga picha mtaani maeneo ya Msikiti wa Mtambani jijini Dar es Salaam. Taarifa zaidi zinasema baada ya waumini hao kumkamata askari huyo walimuhoji kwa muda kisha kutaka kitambulisho chake na kumuamuru afute picha zote alizokuwa akipiga eneo hilo ili wamuachilie kwa usalama wake.
“Kutokana na kuhofia usalama wake alikubaliana nao na kisha kufuta picha zote alizopiga. Walimtaka pia aoneshe kitambulisho na kuhoji ni kwanini anapiga picha wakati yeye ni askari…baada ya kukubaliana na masharti hayo walimuachia,” kilisema chanzo chetu.
“Sisi wenyewe tunashangaa wapiga picha walikuwa wengi wa vyombo mbalimbali vya habari hatujui hawa walijuaje kwamba yule jamaa alikuwa askari na wakati alikuwa amevaa kiraia,” alisema shuhuda mmoja aliyekuwa eneo la tukio.
Jana mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ulinzi na doria iliimarishwa na Jeshi la Polisi ambapo magari na pikipiki za Polisi zikiwa na askari waliojiandaa kutuliza ghasia yalikuwa yakizunguka ikiwa ni kujiandaa kwa kukabiliana na vurugu zozote.
Mitaa kadhaa mwandishi wa mtandao huu alishuhudia askari walio na mabomu ya machozi, huku wakiwa wamevalia vifaa maalumu vya kujikinga na risasi wakizunguka kwenye magari yao maeneo mbalimbali likiwemo eneo la Msikiti wa Mtambani Kinondoni jijini Da rs Salaam, Msikiti wa Mwenge na mingine inayotajwa kama ya wanaharakati. 
Hata hivyo hakuna taarifa za kutokea vurugu zozote.
Taarifa ambazo hazikuthibitishwa zinasema doria ya polisi ililazimika kufanywa baada za kuwepo na taarifa kuwa huenda wafuasi wa Shekhe Issa Ponda wangelifanya fujo kutokana na kutoridhishwa na hatua ya kukamatwa kwa kiongozi huyo kwa tuhuma kadhaa zinazomkabili.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, kuzungumzia kwa kina taarifa hizi hazikuzaa matuna. 

thehabari.com

No comments:

Post a Comment