STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, August 17, 2013

Pambano laMada Maugo, Thomas Mashali utata mtupu

Bondia Thomas Mashali
Bondia Mada Maugo
PAMBANO la kimataifa la kuwania ubingwa wa WBF-Afrika kati ya mabondia Mada Maugo na Thomas Mashali ni utata mtupu baada ya Mashali kutangaza kutolitambua na kusema hayupo tayari kupanda ulingoni kama inavyotangazwa na waandaaji wake.
Akizungumza na MICHARAZO  Mashali alisema anashangaa waratibu wanaotangaza kuwa atapigana na Maugo wakati hawajamalizana naye kwa lolote, huku akitishia kuwaburuza katika vyombo vya sheria kama wataendelea kumtangaza.
Mashali alisema ni kweli kulikuwa na mipango ya kupambanishwa na Maugo, lakini hakuna muafaka wowote uliofikiwa na hivyo anashangaa kutangazwa atapanda ulingoni Agosti 30 kupigana katika pambano la uzani wa kati la raundi 12.
"Sijasaini kokte hivyo silitambui pambano hilo, kwani hata Maugo anayetajwa ndiye mpinzani wangu anatarajiwa kuondoka Agosti 24 kwenda Ghana, ndiyo maana wala sifanyi mazoezi kwa sasa kwa ajili ya shindano lolote, " alisema na kuongeza;
"Nawasiliana na mwanasheria wangu kuchukua hatua dhidi ya watu hao kwani inaweza kuja kuniharibia pambano lisipofanyika kwa kuonekana nimeingia mtini," alisema Mashali alipozungumza kwa njia ya simu na gazeti hili.
Hata hivyo Maugo aliyepo Musoma kwa sasa, alisema anajua pambano lake la Mashali lipo kwa vile alisaini mkataba wa kupigana Agosti 30 kuwania mkanda wa WBF-Afrika na kushangaa kusikia taarifa za mpinzani wake kuukana mchezo huo.
"Japo siwezi kumsemea, lakini mimi nalitambua pambano hilo na nitaanza rasmi mazoezi yangu kwa ajili ya kumtwanga Mashali Jumatatu ijayo. Ni kweli nilikuwa niende Ghana kucheza pambano la kimataifa ila nimeahirisha kwa vile nilishasaini mkataba na waratibu wa pambano la Francis Cheka dhidi ya Mmarekani Phil Williams," alisema.
Maugo alisema yeye hawezi kubweteka na maneno ya Mashali akiamini huenda ni janja yake ya kumfanya aridhike na kutojiandaa na mchezo huo.
Naye Rais wa TPBO-Limited wanaolisimamia pambano hilo, Yasin Abdallah 'Ustaadh' alisema anashangazwa na kauli ya Mashali kuukana mchezo huo wakati alishasaini na kupewa sehemu ya malipo ya awali ya mchezo huo toka kwa waratibu wake.
Ustaadh alisema kama Mashali anamuogopa Maugo na kutaka kulikwepa kijanja pambano hilo anaandike barua na kuiwasilisha TPBO aliposaini mkataba wa awali pia arejeshe kiasi cha fedha alizopewa akitaja Sh. Mil. 2 kati ya 5 walizokubaliana.
"Asitake kutuyumbisha kama anafanya hivyo kwa kumhofia Maugo aseme kwa kuandika barua, ila anachokifanya kinakatisha tamaa mapromota," alisema Ustaadh.
Aliongeza kwa hali kama hii ya Mashali kusaini mkataba na kuchukua malipo ya awali akipendekeza mwenyewe pambano hilo lichezwe raundi 12 badala ya 8 zilizokuwa zimepangwa kisha kuja kulikana ni kuonyesha namna gani mabondia wa Tanzania wasivyojitambua.
"Hii ndiyo inatufanya sisi TPBO kupendekeza kila mara mabondia wetu wapimwe ulevi ili kuepusha usumbufu kama huu, inasikitisha," alisema.
Rais huyo alisisitiza kuwa TPBO na waratibu wa pambano hilo wanatambua kuwa mchezo huo wa Maugo na Mashali upo kama ulivyopangwa licha ya mkwara huo wa Mashali aliyesisitiza hakuna chochote alichokubaliana na waratibu au TPBO Limited.

No comments:

Post a Comment