Waziri wa uchukuzi Prof. Harrison
Mwakyembe amemtaja mshukiwa mmoja wa dawa za kulevya aitwaye Nassoro
Mangunga, lakini mshukiwa huyu pamoja na picha zake alishaandikwa na
gazeti la SANI katika toleo lake la Agosti 7-9, 2013 (toleo la 1042)
pamoja na namna alivyosafirisha mzigo pamoja na akina Masogange.
Isome taarifa yao:
Na Mwandishi Wetu
Unaweza kukimbia lakini huwezi
kujificha. Msemo huu unaonekana kutimia kwa kijana anayedaiwa kuambatana
na watuhumiwa wa dawa za kulevya waliokamatwa Julai 5 mwaka huu nchini
Afrika Kusini, Agness Gerald 'Masogange' (25) na Melisa Edward (24),
kunaswa na gazeti hili.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na
gazeti hili, wasichana hao, Masogange na Melisa walisafiri ndege moja na
kijana anayejulikana kwa jina la Nassoro Mangunga wakitoka Dar es
Salaam kwenda Afrika Kusini, wakisafiri na ndege ya Shirika la Ndege la
Afrika Kusini (SAA), yenye namba SA 189.
Wakiwa katika ndege hiyo Mangunga,
Agness na Melisa walikaa kwenye viti vilivyo jirani kabisa huku Mangunga
akiwa katikati yao, kwani Agness alikaa kiti namba 23B, Mangunga alikaa
kiti namba 23D na Melisa alikaa kiti namba 23A.
Mangunga ambaye ni rafiki mkubwa wa
wanamuziki wa Bongo Flava, Rashidi Abdallah Makwiro 'Chid Benz', Mgaza
Pembe 'M2theP' na Albert Keneth Mangweha 'Mangwair', wakati akisafiri na
mabinti hao walikuwa na jumla ya mabegi tisa kama kumbukumbu za nyaraka
za shirika hilo la ndege zinavyoainisha.
Licha ya nyaraka za kusafirishia mabegi
hayo kuonesha jina la Agness Gerald ambaye ni mpenzi wa Mangunga tangu
mwanzoni mwa mwaka jana, kuwa ndiye aliyelipia mabegi hayo, ila kwenye
sehemu ya anuani ya waraka pepe, imeandikwa ya Mangunga (inahifadhiwa)
ya tovuti ya Gmail.
Aidha, mabegi hayo, yalikuwa na kilo 150
za dawa za kulevya lakini kila mmoja alitakiwa kusafiri na kifurushi
cha kilo ishirini kama mzigo wa mkononi ambao husafiri bila malipo,
hivyo watatu hao kwa pamoja walikuwa na kilo sitini wote kwa pamoja,
hivyi kubaki kilo 90 ambazo walizozilipia Dola za Marekani 94 badala ya
Dola 450.
Mangunga ambaye licha ya kuishi zaidi nchini Afrika Kusini, lakini pia ni mkazi wa maeneo ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Agness na Melisa, walikamatwa Julai 5,
2013 katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Thambo, Afrika Kusini wakiwa na
dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 aina ya Crystal Methamphetamine
zenye thamani ya Sh bilioni 6.8 za Kitanzania, na walipotiwa mbaroni,
walikuwa na mabegi sita tu kati ya tisa waliyokuwa nayo wakati wanapanda
ndege jijini Dar es Salaam.
Inasemekana mabegi hayo matatu
yaliondoka na Mangunga na kutokomea kusikojulikana, jambo linalolifanya
Sani kuzamia zaidi ili kuweka mezani timu nzima inayohusika na mzigo
huo.
Sani
No comments:
Post a Comment