Oscar akishangilia bao lake jioni hii |
Beki Lavren akiitungua Liverpool kwa kichwa |
VIJOGOO vya England, Liverpool leo wamejikuta wakiiangukia pua wakiwa uwanja wao wa nyumbani wa Anfield baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 toka kwa Southampton, na kuipisha Chelsea iliyozinduka leo kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao wa Fulham kukaa kileleni mwa msimamo.
Liverpool iliyokuwa haijaonja chungu ya kipigo katika mechi nne zilizopita za Ligi Kuu ya England ilitunguliwa bao hilo lililofungwa na Dejan Lavren katika dakika ya 53 na kuzima ubabe wake wa kuwafunga wenzake.
Nayo Newcastle United ikiwa nayo nyumbani ilicharazwa mabao 3-2 na Hull City, licha ya kuongoza hadi mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1.
Chelsea muda mchache uliopita imetoka kupata ushindi kwa kuilaza Fulham kwa mabao 2-0, mabao yaliyofungwa na Oscar katika dakika ya 52 na Obi Mikel aliyefunga la pili dakika sita kabla ya pambano hilo lililochezwa Stanford Bridge kumalizika na kumpa afueni kocha Jose Mourinho.
Mechi nyingine za ligi hiyo ya England, Everton ikiwa ugenini imeisulubu West Ham kwa mabao 3-2 nayo Sundeland ikiwa ugenini imetandikwa mabao 3-0 na West Brom na Aston Villa ikiizima Norwich City ikiwa kwake kwa bao 1-0.
Kipute cha ligi hiyo kinatarajiwa kuendelea kesho kwa michezo nne, Arsenal itakuwa ikiufukuzia uongozi wa ligi hiyo baada ya kuenguliwa wiki iliyopita na Liverpool itaikaribisha Stoke City, Manchester City itakuwa nyumbani kuialika Manchester United, Tottenham Hotspur watasafiri hadi nyumbani kwa Cardiff City na Crystal Palace wataikaribisha Swansea City.
No comments:
Post a Comment