Kocha wa JKT, Mbwana Makatta |
KOCHA wa JKT Ruvu, Mbwana Makatta amesema vipigo viwili mfululizo ilivyopewa timu yake na kushushwa kileleni mwa msimamo mwa Ligi Kuu ni makosa yao wenyewe na sasa wanajipanga ili kuweza kuishikisha adabu Simba Jumapili.
Simba na JKT watavaana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam siku ya Jumapili katika mfululizo wa ligi hiyo ya Tanzania Bara itakayoingia raundi ya sita.
Makata alisema kutokana na umuhimu wa mchezo huo wa Jumapili wachezaji wake wataingia leo kambini baada ya mapumziko mafupi, lengo likiwa ni kuhakikisha wanarekebisha makosa yao na kupata ushindi mbele ya Simba.
Kocha huyo alisema vipigo viwili walivyopewa kutoka kwa Ruvu Shooting na Oljoro JKT vilitokana na umakini mdogo waliokuwa nao wachezaji wake kwa vile walitengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao, lakini wakazipoteza.
Makatta anafahamu kwamba ukifanya makosa unastahili kuadhibiwa na anakiri kuwa ndicho kilichowakuta.
"Katika mechi zote tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini wachezaji hawakuwa makini, labda kukosa bahati nako kumetuangusha, hivyo tunajipanga ili Jumapili tuweze kupata ushindi mbele ya Simba," alisema.
Makatta, kipa wa zamani wa klabu za Coastal Union, Tukuyu Stars na Yanga, alisema anajua Simba ni timu kubwa na ngumu, lakini Ruvu haitakubali kupoteza mechi ya tatu mfululizo.
Kocha huyo pia alisema amefurahia matokeo mabaya yaliyozikumba timu zilizokuwa zikiwafukuzia kwa nyuma na kuwafanya wasalie kwenye nafasi ya pili ya msimamo kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
"Kuboronga kwa wenzetu waliokuwa nyuma yetu kumetusaidia kupumua ndiyo maana tunaamini mipango yetu ya kumaliza katika nafasi mbili za juu za msimamo wa ligi mwishoni mwa msimu bado iko sawa," alisema Makatta.
JKT Ruvu ilianza ligi hiyo kwa kasi ikishinda mechi zake zote tatu za awali kabla ya kusimamishwa na ndugu zao Ruvu Shooting na Oljoro na kuwafanya wasalie na pointi 9 wakiiacha Simba kileleni inayoongoza ikiwa na pointi 11.
No comments:
Post a Comment