POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na maiti, iliyokuwa na
pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin tumboni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova alitaja
waliokamatwa kuwa ni Nasri Omari (36), maarufu kama Rajabu Robot na
Mwanaisha Salim( 36), mkazi wa Kigogo Luhanga.
“Kila pipi ina urefu wa sentimita
sita...tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa huko Tabata kuna mtu
mmoja alifariki ghafla muda mfupi baada ya kutoka bafuni kuoga na
tukaamua kulifuatilia tukio hilo” alisema.
Alisema makachero walifika eneo la
tukio, nyumbani kwa Omari na kuhoji hatimaye kugundua uwepo wa maiti
sebuleni ikiwa imelazwa chali katika godoro sakafuni huku akiwa hana
nguo na amefunikwa na shuka.
“Omari ambaye ndiye mmiliki wa chumba
kilichokutwa maiti, alisema marehemu anajulikana kwa jila la Rajabu
Kandunda (43), maarufu kama Mashaka Mabruki” alisema.
Kamishna Kova alisema uchunguzi wa
awali, ulionesha kuwa Kandunda alifika kutoka Mtwara Septemba 21 kwa
maelezo kwamba alikuwa mgonjwa na alikwenda kuchukuliwa na watuhumiwa
hao wawili.
Alisema uchunguzi huo, ulifanywa na jopo
la madaktari wawili na kushuhudiwa na maofisa wa juu wa Polisi na ndugu
wa karibu wa marehemu, ambapo katika uchunguzi huo wa mwili wa
marehemu, tumboni zilikutwa pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin,
zenye thamani ya mamilioni ya fedha.
“Zipo taarifa zinazoonesha kwamba
alikuwa ni mhalifu mzoefu wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kwani
kabla ya kurudi Tanzania alikuwa akitumikia kifungo nje ya nchi barani
Asia” alisema.
Kova alisema uchunguzi zaidi unafanyika
ili kujua mtandao mzima wa usafirishaji wa dawa hizo, ambao umemhusisha
marehemu. Alisema wote watakaobainika kuhusika, watakamatwa na
kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha alisema baada ya upekuzi, marehemu
huyo alikutwa na vielelezo vingine, ikiwemo fedha za Kenya Sh 700, Dola
za Marekani 100 na fedha ya Ushelisheli.
Alisema operesheni ya kukamata dawa za
kulevya, inaendelea. Aliomba raia wema kuendelea kutoa taarifa za dawa
hizo, kwani zina madhara makubwa kwa wananchi, hasa vijana.
No comments:
Post a Comment