Uhuru Seleman akiwa na taji la ubingwa la Ligi Kuu alipokuwa Simba |
Uhuru ambaye ni mwenyeji wa Mbeya, alisema wiki iliyopita Coastal ilipoenda kuumana na Mbeya City alishangazwa na namna wakazi wa mkoa huo walivyoungana pamoja na kuishangilia timu yao mwanzo mwisho kitu alichodai hajawahi kukiona Tanga na kuwataka 'Wagosi wa Kaya' kuzinduka.
Kiungo aliyewahi kuzichezea Mtibwa Sugar, Simba na Azam, alisema kwa namna mashabiki wa mkoa Mbeya wanavyoungana na kuzisahau kabisa Simba na Yanga inawatia moyo na kuwapa nguvu wachezaji wa timu hiyo kujituma uwanjani.
"Huwezi amini ukiwa Mbeya husikii habari za Simba na Yanga wao na Mbeya City na Prisons, kitu ambacho nilikuwa napenda kuwaomba mashabiki wa soka wa mkoa wa Tanga kuiga jambo hilo na kuwa na uzalendo kwa timu zao na hasa Coastal Union iliyopo Ligi Kuu," alisema.
Alisema sapoti wanayopewa wachezaji wa Mbeya City inawatia moyo na kupata nguvu ya kuipigania timu yao kuweza kuwa na matokeo mazuri licha ya ugeni wake katika ligi hiyo inayozidi kushika kasi.
"Uzalendo wa namna hiyo wa kuziunga mkono timu za nyumbani husaidia kuwatia nguvu wachezaji badala ya utamaduni wa mashabiki kugawanyika kwa unazi wa Simba na Yanga na kuzisahau timu zao ambazo zinawapelekea mechi kubwa na kuziona timu wanazoziota," alisema Uhuru.
Kiungo huyo na wachezaji wenzake watakuwa uwanja wa Mkwakwani Tanga kesho kwa ajili ya kuwakabili Azam katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu hizo zote zinatokea Mbeya walipoumana na wenyeji wao Mbeya City na Prisons na kuambulia sare ya bao 1-1 kila moja.
No comments:
Post a Comment