STRIKA
USILIKOSE
Saturday, November 30, 2013
CHADEMA YAAMUA KUFUNGA MDOMO SAKATA LA ZITTO
HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa mjadala kuhusu viongozi wake waliovuliwa nyadhifa zao kwa madai ya kukisaliti chama umefungwa.
Viongozi waliovuliwa nyadhifa zao ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, aliyevuliwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo, aliyevuliwa ujumbe wa Kamati Kuu (CC) na Samson Mwigamba, aliyevuliwa uenyekiti wa Mkoa wa Arusha.
Kauli ya kufunga mjadala huo ulioshika kasi kwa takribani wiki moja sasa, ilitangazwa jana na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk. Slaa alisema mjadala huo umefungwa, na tayari barua za mashitaka 11 kwenda kwa watuhumiwa zimeshatumwa.
“Nataka niwaambie wana CHADEMA wote wanaotumia mitandao na njia nyingine za mawasiliano kwamba mjadala huo sasa umefungwa, hatutaki kusikia, kuona mwanachama yeyote anauendeleza, lakini tutajibu tu pale itakapoonekana kuna upotoshaji,” alisema Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kazi iliyobaki ni kwa watuhumiwa kujibu mashitaka yao ndani ya siku 14 na hatma yao itajulikana kwenye kikao cha Kamati Kuu (CC).
Dk. Slaa ambaye amepata kuwa mgombea urais wa CHADEMA mwaka 2010 na kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano, alisema kuna mambo mengi mazito ya kujadili kuliko hilo la mzozo wa Zitto na wenzake.
“Tumekumbwa na tatizo la umeme hapa ambao hatujui chanzo, kuna wenzetu wanaendelea kupigwa na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji, hatuwezi kuendelea na malumbano ambayo hayana tija, CHADEMA ni chama makini na bado kiko imara,” alisema Dk. Slaa.
Kauli ya Dk. Slaa itahitimisha mjadala huo ambao tangu watuhumiwa hao walipotangazwa kuvuliwa madaraka, kumekuwa na majibishano kati ya viongozi wa CHADEMA na watuhumiwa hao.
Mara baada ya mkutano na waandishi wa habari wa kutangaza uamuzi wa kuwavua madaraka viongozi hao, Zitto na Dk. Kitila kwa mara ya kwanza walijibu mapigo katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Zitto na Kitila walitaja sababu walizodai ndizo zimewafanya kuvuliwa nyadhifa zao, ikiwemo suala la ukaguzi wa hesabu za fedha za ruzuku inayotolewa kwa vyama vyenye wabunge, kikiwemo CHADEMA.
Zitto alidai kwa muda mrefu amekuwa akizushiwa kupokea rushwa na kukisaliti chama, na kwamba hatoki ndani ya chama hicho kwani nusu ya maisha yake tangu alipojiunga akiwa na miaka 16, hadi sasa ana miaka 37, maisha yake yapo CHADEMA.
Kutokana na maelezo hayo ya Zitto na Kitila, CHADEMA juzi walilazimika kuitisha mkutano na kudai kuwa viongozi hao waliovuliwa madaraka, walishindwa kusema ukweli mbele ya waandishi wa habari wiki iliyopita wa kile kilichowafanya wavuliwe nafasi zao.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, alisema Zitto na Dk. Kitila hawakusimamishwa nyadhifa zao kwa masuala ya PAC, uchaguzi wa mwaka 2010, wala kutoshiriki kwenye operesheni za chama au sababu nyingine, na kwamba walitaja sababu hizo ili kupotosha tuhuma zinazowakabili kwa jamii.
“Walichokifanya kina Zitto na Kitila ni “Diversion” (kubadili mwelekeo) wa mashitaka yao yanayotokana na waraka wa kihaini wa mabadiliko, ambao ni kinyume na katiba, kanuni na maadili na itifaki ya chama,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa CHADEMA ina mwongozo wa uchaguzi uliopitishwa na Kamati Kuu, na Zitto na Kitila wanaufahamu ingawa haijulikani ni kwanini wao walienda kinyume na mambo yanayojadiliwa katika Kamati Kuu.
Aidha, Lissu alieleza kuwa Dk. Kitila anapotosha umma kwa kauli yake kuwa Kamati Kuu haina mamlaka ya kumvua nafasi yake ya ujumbe wa Kamati Kuu maana amechaguliwa na Baraza Kuu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment