Jeshi la polisi mkoani Arusha limemshikilia na kisha kumwachia
“chapchap” mtoto wa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro
na mfanyabiashara maarufu nchini,Oscar Themi kwa kosa la kumpiga
risasi ya kichwa mhudumu wa bar ya Empire iliyopo eneo la Shoprite
jijini Arusha.
Mtuhumiwa huyo ,Dereck Themi alishikiliwa na polisi mwishoni mwa wiki
iliyopita mara baada ya kutofautiana na mhudumu huyo wakati alipompatia
bili ya vinywaji aliyokuwa akitumia ndani ya bar hiyo kabla ya
kumtandika risasi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa
mnamo novemba 29 mwaka huu majira ya saa 7.30 usiku mtoto huyo wa kigogo
alimfyatulia risasi mhudumu huyo aliyetambulika kwa jina la Witness
Erasto wakati alipompatia bili ya vinywaji.
Mashuhuda walidai kuwa kulitokea na hali ya tofauti kati yao ambapo
Themi alikubali kulipa bili hiyo ambapo alichukua fedha na kisha
kumwekea katika matiti yake na ghafla kuchomoa bastola yake na kisha
kumtandika eneo la kichwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa mara baada ya tukio
hilo ndipo mtuhumiwa alijaribu kukimbia nje ya bar hiyo kuelekea usawa
wa eneo la maegesho la magari lakini kabla hajafika alifyatua risasi
nyingine zaidi ya tano hali iliyopelekea tafrani katika eneo la
Shoprite.
Hatahivyo,taarifa hizo zimedai kuwa askari mmoja aliyekuwa akilinda
benki ya Exim iliyopo ndani ya eneo hilo la Shoprite alimvizia kimafia
na kisha kumnyang”anya bastola hiyo mtuhumiwa kabla ya kuwataarifu
polisi waliofika eneo hilo na kisha kumfikisha katika kituo kikuu cha
polisi cha kati.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa katika kituo hicho na kisha kukabidhi bastoa
hiyo pamoja na maganda matano ya risasi ambapo baada ya muda aliwasili
mdogo wake aliyetambulika kwa jina la Bernad Themi aliyechukua mali zake
na fedha.
Akihojiwa na gazeti hili majeruhi wa tukio hilo Erasto alisema kuwa
hawezi kuongea chochote kwa kuwa hali yake ni sio nzuri lakini
alipotafutwa mmiliki wa bar hiyo,Tumaini Ulomi alikiri kutokea kwa tukio
hilo na kusema kuwa tayari wameshafungua mashtaka mbalimbali ikiwemo
hasara aliyoipata siku ya tukio.
Mmiliki huyo alisema kuwa mara baada ya milio ya risasi kuanza kurindima
ndani ya bar yake wateja mbalimbali wakiwemo watalii walitokomea
kusikojulikana bila kulipa hali ambayo imemtia hasara kubwa.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas alikiri kutokea
kwa tukio hilo na kusema kwa kifupi kwamba bado wanafanya uchunguzi wa
kina kabla ya kulifikisha suala hilo mahakamani.
Credit :libeneke la
kaskazini
No comments:
Post a Comment