Kocha wa zamani wa Yanga na Bandari Mtwara, Kennedy Mwaisabula (kushoto) akiwa na viongozi wenzake wa Tukuyu Stars Family |
Mwaisabula, alitangazwa jana na TFF baada ya Rais wake Jamal Malinzi kutangaza kamati mbalimbali ikiwemo kumteua Pelegrinius Rutahyuga kuwa mshauri wake kwa upande wa masuala ya ufundi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika hafla maalum iliyoandaliwa na wadhamini wakuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kampuni ya Bia nchini (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro, Malinzi alisema jopo hilo litakutana kwa siku tatu Desemba 6-8, mwaka huu visiwani Zanzibar kupanga mkakati wa kuonyesha jinsi Tanzania inavyoweza kushiriki michuano ya Afcon itakayofanyika 2015 nchini Morocco.
Malinzi alisema jopo hilo litaongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali mstaafu Idd Kipingu, huku wengine wanaounda jopo hilo linalohusisha pia makocha wakiwa ni Mshindo Msolla, Peter Mhina, Ayoub Nyenzi, Abdallah 'King' Kibaden, Rutahyuga (Katibu wa Jopo), Kidao Wilfred, Salum Madadi, Juma Mwambusi, Ken Mwaisabula, Fred Minziro, Meja Abdul Mingange, Ally Mayay, Boniface Mkwasa na Dan Korosso.
"Wajumbe wengine watatu wa jopo hili wanatoka Chama cha Soka Zanzibar (ZFA). Ni memteua Pelegrinius Rutahyuga kuwa mshauri wa rais (ufundi). Mshauri wa rais (utawala) nitamteua baadaye," alisema Malinzi.
Aidha, Malinzi alisema Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana Desemba 22, mwaka huu kujadili masuala mbalimbali yakiwamo ya uteuzi wa wajumbe wa kamati za kisheria na mgogoro wa uongozi wa Klabu ya Simba.
TBL WAMPONGEZA
Katika hatua nyingine, uongozi wa TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro, umempongeza Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa rais wa shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema jana katika hafla hiyo, uongozi wa kampuni yao utaendelea kushirikiana na TFF kuendeleza soka la Tanzania.
No comments:
Post a Comment