Baadhi ya makocha ambao wanatarajiwa kuivaa TASWA, Bakar Idd (kushoto) Seleman Matola watatu toka kushoto, anayemfuata ni Mwalala wakiwa na Shafii Dauda 'Fundi' (wa pili kushoto) |
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, Benard Mwalala na makocha wasaidizi wa Simba na Azam, Kally Ongalla na Seleman Matola ni baadhi ya wachezaji wanaotarajiwa kuunda timu ya Makocha itakayocheza mchezo wa kirafiki na TASWA FC katika kusindikiza tuzo za Makocha wa Soka Tanzania inayotarajiwa kutolewa Machi 8, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na MICHARAZO jijini, afisa mtendaji wa tuzo hiyo, Fredrick Luunga alisema mchezo huo pia utatumika kumuenzi aliyekuwa mweka hazina na mchezaji wa Taswa FC, Sultan Sikilo na aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba SC, James Kisaka, waliofariki dunia hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Luunga alisema maandalizi kwa ajili ya tuzo hiyo yanakwenda vizuri na kwamba anaamini mchezo huo utakuwa chachu kwa kuwa pia utawakutanisha makocha na waandishi wa habari za michezo na kupata fursa ya kubadilishana mawazo.
“Hili ni wazo jipya ambalo tumelipata tumeona ni vema kuandaa mchezo wa kirafiki kati ya timu ya makocha na Waandishi wa habari za michezo nchini kabla ya utoaji wa tuzo ili kuleta changamoto zaidi”, alisema.
Afisa huyo alisema mchezo huo unatarajiwa kuchezwa mapema siku hiyo ya utoaji wa tuzo katika uwanja utakaopangwa baadaye.
Mbali ya Mwalala, Matola na Ongala, makocha wengine wanaotarajiwa kuunda kikosi cha timu hiyo ni Juma Pondamali ‘Mensah’, Idd Pazi ‘Father’, Patrick Mwangata, Charles Boniface Mkwasa, Fred Felix Minziro, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, Charles Kilinda, Amri Said, Adolf Rishard, Mecky Maxime, Joseph Lazaro, Bakari Shime, John Tamba, Jackson Mayanja, Mrage Kabange na Ken Mwaisabula.
Wakati huo huo, luunga alisema zoezi la kuwapigia kura makocha ili waweze kushinda tuzo hizo limeshaanza na kwamba wadau wa soka wanatakiwa kuwachagua makocha wanaoona wanastahili kupata tuzo.
Luunga alisema namna ya kupiga kura, mdau wa michezo anatakiwa kuandika katika simu yake neno sokafasta acha nafasi kisha jina la kocha yeyote na tuzo anayostahili kupata kisha itumwe kwenda 15678.
Tuzo zinazotarajiwa kutolewa siku hiyo ni kocha bora wa mwaka, kocha bora wa makipa, kocha mkongwe mwenye mafanikio, kocha bora chipukizi, kocha bora wa kike, kocha bora wa kigeni, kocha wa kigeni aliyewahi kupata mafanikio makubwa na kocha bora Mtanzania anayefundisha nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment