STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 19, 2014

Olaba ampotezea Maguri, adai anawaamini vijana alionao

http://images.supersport.com/2014/1/AFC-Tom-Olaba-1-300.jpg
Kocha Tom Oloba

Elias Maguri aliyetimkia Umangani
KOCHA mpya wa Ruvu Shooting, Mkenya Tob Olaba amempotezea kiaina mshambuliaji nyota wa timu hiyo aliyetimkia Umangani, Elias Maguri, akisema asingependa kumjadili kwa sababu anawaamini vijana alionao watambeba kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara inayoanza duru la pili wikiendi ijayo.
Pia alisema kikosi chake hakitacheza mchezo wowote kwa sasa badala yake atautumia muda uliosalia kabla ya kuanza kwa duru la pili la ligi kurekebisha makosa aliyoyaona kwenye michezo mitatu ya kirafiki waliyocheza ili Alhamis waifuate Prisons-Mbeya wakiwa kamili gado.
Akizungumza na MICHARAZO, Olaba aliyetua katika klabu hiyo kuziba nafasi ya Charles Boniface aliyehamia Yanga kama kocha msaidizi, alisema hapendi kuwazungumzia Maguri na Ally Kani waliotimikia nje ya nchi kwa sababu hajawahi kuwanoa tangu atue kikosini hivyo hajui ubora na udhaifu wao.
Olaba alisema kadhalika huwa ana kawaida ya kumuamini mchezaji yeyote anayejituma na kujitambua hivyo vijana aliowakuta na kuanza kujipanga upya pamoja anawaamini watafanya kazi zote kwa manufaa ya Ruvu hivyo hakuna haja ya wadau wa Ruvu kuwafikiria akina Maguri.
"Sijawahi kumuona wala kujua uwezo alionao Maguri au huyo Kani, hivyo sitaki kuwajadili kwa sasa kwa vile nawaamini vijana nilionayo wanaweza kazi na kuisaidia Ruvu, kwangu kila mchezaji ana nafasi sawa mradi tu wajitume na kuisaidia timu," alisema.
Alisema kuanzisha mjadala wa akina Maguri klama wameacha pengo au la ni kutaka kuiyumbisha timu kwa kuwakatisha tamaa wachezaji waliopo aliowasifia kuwa ni wakali na waliomkuna wakimpa matumaini ya kumfikisha kule anakopataka kama kocha mkuu wa timu hiyo.
Kuhusu maandalizi ya mechi yake ya fungua dimba itakayochezwa dimba la Sokoine Mbeya, Olaba alisema hatacheza tena mechio yoyote ya kujipima nguvu kwa sasa kwa vile walizocheza zinatosha na badala yake atajikita katika kurekebisha makosa aliyoyagundua ili kwenda kuivaa Prisons wakiwa wamekamilika.
"Tutakuwa tukirekebisha kila baada ya mchezo mmoja wa Ligi Kuu, kwa sasa namalizia dosari chake hasa suala la pumziko na umakini kwa wachezaji ili tuende kuivaa Prisons tukiwa na uhakika wa kuzoa pointi zote tatu kabla ya kuangalia mechi itakayofuata baada ya hapo," alisema Olaba kocha wa zamani wa Mtibwa na klabu kadhaa za nchini Kenya ikiwamo timu ya taifa, Harambee Stars.
Elias Maguri ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa klabu yake ya Ruvu Shooting akiwa na magoli 9 kwenye Ligi Kuu nyuma ya kinara, Amissi Tambwe wa Simba mwenye mabao 10, na kukosekana kwake kunaelezwa kama kunaweza kuiadhiri timu hiyo katika mechi za duru la pili chini Olaba.

No comments:

Post a Comment