Na Peter Mwenda, Mkuranga
MWENYEKITI wa Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA), Profesa Penina Mlama ametoa wito kwa wasanii kuchangamkia
kuchangia ujenzi wa nyumba unaratibiwa na Mtandao wa wasanii Tanzania (SHIWATA)
ili kujiandalia makazi.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi
wa ujenzi wa nyumba za wasanii katika kijiji cha Mwanzega, wilaya ya Mkuranga
mkoani Pwani, Profesa Mlama alisema makazi ni sehemu ya maisha ya binadamu
hivyo wasidharau mradi huo ni faida kubwa kwao.
Alisema nyumba ambazo ameziona ni
nzuri, imara na zinauzwa bei ya chini ambayo huwezi kuzipata sehemu nyingine
yoyote nchini Tanzania na kuongeza kuwa kujenga kwa lengo la kuishi pamoja
kunatoa fursa ya wasanii kubuni njia nyingine ya kuanzisha miradi mbalimbali.
Profesa Mlama alitaka SHIWATA isikate
tamaa bali iendelee kuwashawishi wasanii wajiunge na kuchangia ujenzi wa nyumba
ili baadaye wasitafute visingizio kuwa hawakupewa fursa hiyo.
Naye Katibu Mtendaji wa
BASATA,Godfrey Mngereza alisifu SHIWATA kubuni njia ya kuwasainia wasanii kupata
makazi na kuahidi kuwa baraza hilo litatoa ushirikiano na kutoa ushauri kila
unapohitajika.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib
alisema mpango wa ujenzi wa nyumba za wasanii utaendelea kote nchini na
kuwataka wasanii waungane kufanya kazi zao kwa pamoja.
Alisema mpaka sasa nyumba 38
zimekabidhiwa kwa wasanii waliochangia ujenzi katika kijiji cha Mwanzega
Mkuranga na nyingine 21 zinatarajiwa kukabidhiwa Machi mwaka huu.
SHIWATA mbali ya kusimamia ujenzi wa
nyumba za wasanii inasimamia matamasha ya wasanii wachanga (Underground) kuendesha
makongamano ya kupambana na kuzuia dawa za kulevya na kutoa elimu na maadili kwa
wasanii.
No comments:
Post a Comment