Babi (kushoto-mbele) akiwa na kitambaa cha unahodha |
Babi alipewa unahodha huo wiki iliyopita alipoingoza timu hiyo katika mchezo dhidi ya 'vibonde' wa ligi hiyo Perlis na kupoteza mchezo huo wa ugenini kwa kulala mabao 2-1.
Kiungo huyo wa zamani wa Taifa Stars, aliiambia MICHARAZO kuwa nidhamu na kiwango bora cha soka alichokionyesha tangu atue katika timu hiyo ndicho kilichofanya apewe cheo hicho na kusema anamshukuru Mungu.
"Ninajisikia fahari kupewa cheo hicho baada ya viongozi na wachezaji kuridhika na uwezo wangu uwanjani na nidhamu kubwa niliyonayo ni furaha kwangu hasa ikizingatiwa nipo ughaibuni," alisema Babi.
Kuhusu mechi yao ya Ijumaa, Babi alisema walifungwa kimchezo katika pambano hilo la ugenini lililochezwa kwenye uwanja wa Darul Aman mjini Alor Setar, likiwa pambano lao la tatu mfululizo kupoteza. Wako katika nafasi ya tisa wakiwa na pointi nne tu.
"Tumefungwa kimchezo na kwa muda kulikuwa na mgogoro wa kiuongozi ambao kwa sasa umeisha na tunajipanga kwa mechi yetu ya Ijumaa hii tutakayocheza nyumbani," alisema Babi, nahodha wa zamani wa Yanga.
UiTM itaumana na DRB-Hicom katika mechi ambayo Babi ametamba kwamba timu yake wataibuka na ushindi katika mechi hiyo itakayochezwa uwanja wa Mini UiTM, katika mji wa Shan Alam.
Babi aliyewahi kuzichezea pia Mtibwa Sugar, Azam na KMKM kabla ya kutimkia Malaysia alikosaini mkataba wa mwaka mmoja, alisema ligi ya nchi hiyo ni ngumu na imejaa ushindani tofauti na alivyofikiria mwanzoni.
No comments:
Post a Comment