KOCHA
Mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari amesema morali ya wachezaji
wake ipo juu kwa ajili ya mechi dhidi ya Afrika Kusini (Amajimbos)
itakayochezwa leo.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi
ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17
itafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es
Salaam kuanzia saa 10 jioni.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa
habari kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam, Kocha Hababuu
amesema nia ya kikosi chake ni kuhakikisha wanafika kwenye fainali za
Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Niger.
“Tunaiheshimu Afrika
Kusini, lakini hatuiogopi. Morali ya wachezaji ipo juu na wanajiamini.
Kimsingi wanajua kuwa hii ndiyo njia ya wao kutokea kwenye mpira wa
miguu, kwa hiyo lengo ni kushinda,” amesema Kocha Hababuu.
Naye Kocha wa
Afrika Kusini, Molefi Ntseki amesema anaziheshimu timu za Tanzania, na
changamoto aliyonayo ni kuhakikisha kuwa anashinda mechi hiyo kwani mara
ya mwisho kwa timu yake kushiriki fainali za Afrika ilikuwa miaka sita
iliyopita. Kiingilio katika mechi hiyo ni sh. 2,000 na tiketi
zitapatikana uwanjani kwenye magari maalumu.
No comments:
Post a Comment