THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Website : www.ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425 |
PRESIDENT’S OFFICE,
STATE HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa
Abbas Kandoro kuomboleza vifo vya watu 10 vilivyotokea Mbalizi, Mkoani
Mbeya tarehe 29 Agosti, 2014 baada ya basi dogo la abiria aina ya Toyota
Hiace maarufu kama Daladala Na. T 237 BFB kugongana na lori aina ya
Tata Na. T 158 CSV. Katika ajali hiyo, watu saba wengine walijeruhiwa
na kukimbizwa hospitali kwa matibabu.
“Nimesikitishwa
na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 10 na wengine saba
kujeruhiwa katika ajali hii iliyotokea siku chache baada ya ajali
nyingine kutokea Mkoani Tabora iliyoua watu 19 na wengine 81
kujeruhiwa”, amesema Rais katika salamu zake.
Rais
Kikwete amesema mfululizo wa ajali hizi unaonyesha dhahiri kuendelea
kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa umakini miongoni mwa madereva, hivyo
jitihada zaidi zinatakiwa kufanywa kusimamia kikamilifu Sheria ya
Usalama Barabarani na kufuatiliwa kwa karibu kwa mienendo ya
wanaoendesha vyombo vya moto, ili ajali hizi ziweze kupunguzwa na hata
kudhibitiwa kabisa katika barabara zetu.
“Naomba
upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana
na ajali hiyo, na kupitia kwako naomba unifikishie salamu zangu za pole
kwa wafiwa wote kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao”Ameongeza.
Rais
Kikwete amesema anatambua machungu waliyo nayo wanafamilia, ndugu na
jamaa wa watu waliopoteza maisha yao kwenye ajali hiyo, lakini anawaomba
wote wawe wavumilivu na wenye subira wakati huu wanapoomboleza vifo vya
ndugu na jamaa zao.
“Ninawaombea
kwa Mola majeruhi wote wa ajali hiyo waweze kupona haraka na kurejea
katika hali zao za kawaida ili waweze kuungana tena na familia, ndugu
na jamaa zao”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika salamu zake.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
31 Agosti,2014
No comments:
Post a Comment