SULEIMAN MSUYA
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHGG) imesema asilimia kubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu hapa nchini unaanzia pale mtu anapokamatwa na vyombo vya dola kwenye mahojiano pamoja na mahabusu.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Kisheria (CHGG) Nabor Assey wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam.
Assey alisema utafiti unaonyesha kuwa wengi wao wanakamatwa pasipo utaratibu, kudhalilishwa, kuteswa, kubambikiwa kesi, kuwekwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani na kuwepo mazingira magumu ya dhamana jambo linalokiuka haki za binadamu zilizoainishwa katika ibara ya12 mpaka 24 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na sheria zingine za nchi na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa.
Mkurugenzi huyo utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 50 ya watu wanaoshikiliwa maeneo mbalimbali nchini ni mahabusu ambao ama wanasubiri kufikishwa mahakani au kesi zao zinaendelea katika mahakama mbalimbali bado hawajahukumiwa.
“Napenda kuweka wazi kuwa hii ni Idara huru ya Serikali tunachokisema hapa ni katika juhudi za kusaidia serikali kutatua changamoto ambazo zinaikabili jamii yake hasa katika masuala ya haki za binadamu” alisema.
Assey alisema ni wazi kuwa vyombo vya dola hasa jeshi la polisi limekuwa likishutumiwa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu hali ambayo inahitaji elimu zaidi ambayo inaweza kusaidia kutatua tatizo hilo.
Alisema ni vema dhana halisi ya jina la polisi (Pilice Force) kubadishwa na kuwa (Police Service) ili kuwapatia uelewa kuwa wanapaswa kutoa huduma na sio kutumia nguvu zaidi kama njia ya kukabiliana na tatizo.
Mkurugenzi huyo alisema pia kuna mapungufu katika mfumo wa sheria za jina za Tanzania akitolea mfano ibara ya 13(6) (e) ya Katiba ya Tanzania ya 1977 inakataza utesaji kwa watuhumiwa na kuelekeza mamlaka za nchi kutunga sheria kwa minajili hiyo.
Alisema bado kuna upungufu katika sheria kwani kifungu cha 29 cha sheria ya ushahidi sura ya 6 ya sheria za Tanzania kinakata ushahidi uliopatikana kwa shinikizo la aina yoyote kutumika kama ushahidi halali mbele ya mahakama.
Assey alisema pamoja na sheria hizo kuonyesha ukatazo bado hazijaonyesha ni hatua gani atachukuliwa mtumishi yeyote ambaye atabainika kufanya vitengo vinavyokiuka haki za binadamu.
Alisema Tume yao ipo katika mchakato wa kuhakikisha kuwa vyombo vya usalama vinapatiwa elimu yakutosha juu ya nini majukumu yao pale ambapo wanamshikilia mtu ambaye amefanya kosa.
Mkurugenzi huyo alisema jitihada hizo zinatakuwa zikishirikisha wananchi hasa kwa kudai haki zao ambazo hazipo kisheria ambao wanaonekana kuwa waathirika wakubwa kutokana na vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment