Amissi Tambwe (wa Tano toka Kulia) akichuana kwenye mechi yao na Ruvu Shooting ambapo alilalamika kubaguliwa na kukabwa na George Assey (wa kwanza kulia) katika pambano lililoisha kwa sare ya 0-0 |
WIZARA
ya Habari Utamaduni na Michezo imeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), kutoa adhabu kwa timu ya Ruvu Shooting kutokana na kitendo cha
ubaguzi kilichofanywa na wachezaji wa timu hiyo dhidi ya mshambuliaji wa
Yanga kutoka nchini Rwanda, Amissi Tambwe.
Akizungumza
na Ripota wa Globu ya Jamii, Naibu Waziri wa Habari, Juma Nkamia
amesema kuwa TFF isikae kimya kutokana na matamshi ya udhalilishaji juu
ya Tambwe na kuiagiza TFF kuchukua hatua za kinidhamu haraka iwapo
itathidibitika mshambuliaji huyo alitolewa maneno hayo ya udhalilishaji
ili iwe fundisho kwa wengine.
"Hakuna
nchi yoyote duniani inayopenda vitendo vya ubaguzi, kitendo ambacho
upendi kufanyiwa usimfanyie mwenzie, nimesikia malalamiko ya Tambwe kama
ni kweli Ruvu Shooting wamemuita mkimbiza wajue sio kitu kizuri tena
wale ni jeshi, nadhani wanajua madhara ya vita.
"Wenzetu
Burundi hawakupenda kuingia vitani, hakuna nchi yoyote inayopenda kuwa
vitani, vita ni mbaya hata hapa inaweza kutokea, ni jambo la kumshukuru
Mungu mpaka leo mna amani, uwezi kujua mtu unayemwambia ameumia kiasi
gani na hiyo vita ni ndugu wangapi au marafiki wangapi amewapoteza sio
kitu kizuri, naiagiza TFF ishugulikie suala hili kwa kuchukua hatua za
haraka."alisisitiza Nkamia.
Kauli
ya Nkamia imekuja siku moja baada ya Tambwe kulalamikia kitendo cha
kuitwa mkimbizi na wachezaji wa Ruvu Shooting wakiongozwa na George
Michael ikiwa ni pamoja na kumkaba nusura wamtoe roho.
"Maneno
makali waliyonitamkia yananiuma sana roho hadi sasa, wameniita
mkimbizi, eti nimekimbia vita nyumbani Burundi, vita hata hapa inaweza
kutokea, hakuna anayependa mabaya kama hayo yatokee, kumwambia mtu
haujui kapoteza ndugu wangapi, si sahihi kabisa, cha kushangaza wale ni
wanajeshi lakini hawaonyeshi kuwa wanajua athari za vita." kauli
iliyotolewa na Tambwe jana.
Hata
hivyo Chama cha Waamuzi nchini (FRAT), kimetangaza kumfungia mwamuzi wa
kati wa mchezo huo Mohamed Theofil, huku ikiwaweka kwenye uchunguzi
waamuzi wasaidizi Michael Mkongwa na Yusuf Sekile.
Mwenyekiti
wa FRAT, Salum Chama aliiambia Globu ya Jamii kuwa wamefikia uamuzi wa
kumsimamisha Theofil baada ya ripoti ya Kamisaa kuonyesha kuna mapungufu
yaliyofanywa na mwamuzi huyo ambaye katika mchezo huo uliomalizika kwa
suluhu, alishindwa kumudu mchezo kutokana na rafu za mara kwa mara
kitendo kilicholazimu mpira kusimama kila dakika.
"Ripoti
ya kamisaa imeonyesha kuna udhaifu mkubwa uliofanywa na mwamuzi, kamati
yangu imemfungia kupisha uchunguzi, na bado tunaendelea na uchunguzi
pia kwa waamuzi wasaidizi, kikao cha kamati yangu kitakaa Februari 6
kuwajadili na kuangalia adhabu stahiki itakayofaa.
"Kitendo
kinacholalamikiwa sana ni kile cha Tambwe, na ni kweli kila mtu ameona,
hata kama ripoti ya kamisaa isingesema tungechukua hatua kwa sababu
wapo viongozi wa TFF walioona, tunachunguza ripoti ya mechi asesa,
kamisaa,"alisema Chama.
Hata
hivyo, Chama alisema kuwa hawafanyi kazi kwa shinikizo la Yanga ambao
waliwapa mpaka Jumamosi wawe wameshatoa adhabu kwa waamuzi wa mchezo wao
na Ruvu Shooting la sivyo watagomea Ligi.
Kwa hisani ya Michuzi blog
No comments:
Post a Comment