Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Amos Makalla atakayekuwa mgeni rasmi katika pambano la ngumi la kuwania ubingwa wa UBO Mabara kati ya Francis Cheka na Karama Nyilawila |
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni Vijana na Michezo, Amos Makalla anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa pambano la kimataifa la kuwania ubingwa wa Mabara wa UBO kati ya mabondia Francis Cheka na Karama Nyilawila.
Pambano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam Septemba 29, na waratibu wa mchezo huo, kampuni ya Afrika Kabisa Entertainment wamesema Waziri Makalla ndiye atakayemvisha taji mshindi.
Promota Robert Ekerege, aliiambia MICHARAZO kwamba tayari amehakikishiwa na Waziri Makalla kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo la Super Middle la raundi 12 amblo litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
"Mgeni rasmi katika pambano letu kati ya Cheka na Nyilawila atakuwa Naibu Waziri wa Michezo, Amos Makalla, na kila kitu kimekamilika katika maandalizi ya pambano hilo," alisema Ekerege.
Ekerege alisema mbali na Waziri Makalla, pia siku ya pambano hilo litahudhuriwa na Mlezi wa mchezo wa ngumi nchini, Suleiman Kova ambaye ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, katika kunogesha pambano hilo mabondia kadhaa karibu 10 watapanda ulingoni kuwasindikiza akina Cheka kwa kucheza michezo ya raundi sita kila moja na wa watasindikiza na burudani toka Mashujaa Band.
"Mashujaa Band ndio watakaosindikiza michezo hiyo yote ambayo itakuwa na ulinzi wa kutosha ili kudhibiti vitendo vyote vya kihuni ambavyo vinaweza kutuharibia," alisema Ekerege.
Mwisho
No comments:
Post a Comment