Med Sebyala wa Uganda akiwa na taji lake la ubingwa wa Uganda |
Thomas Mashali wa Tanzania akiwa na ubingwa wake wa TPBO |
BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Thomas Mashali anatarajia kuzidunda na Mganda Med Sebyala katika pambano la kuwania taji la Afrika Mashariki siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Pambano hilo la uzati wa kati la raundi 10 limepangwa kufanyika Oktoba 14 kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese Dar es Salaam.
Mratibu wa pambano hilo litakalosimamiwa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO, Regina Gwae alisema tayari wameshamalizana na mabondia hao kwa ajili ya pambano hilo la kimataifa.
Regina, alisema pambano hilo ni fursa nzuri kwa Mashali anayeshikilia ubingwa wa Taifa wa TPBO kujitangaza kimataifa iwapo atafanikiwa kumnyuka Sebyala.
“Huwezi kwenda nje kama ndani hufanyi vizuri na huwezi kwenda Ulaya, iwapo unashindwa kutamba Afrika Mashariki, hivyo tumeona tumpe Mashali mchezo huu ili akifanya vyema aweze kuvuka mipaka ya sasa, "alisema Regina.
Regina alisema ana matumaini mpambano huo utakuwa mzuri na utakaovutia kutokana na ukweli mabondia wote wawili wana sifa zinazofanana waking'ara ndani ya nchi zao.
Alisema Sebyala ni mmoja wa bondia wazuri waliowasumbua baadhi ya nyota wa ngumi nchini kama Rashid Matumla na Francis Cheka aliowahi kuja kucheza nao hapa nchi katika mechi za zisizo za ubingwa.
Mratibu huto aliwaomba wafadhili wajitokeze kwa ajili ya kudhamini mchezo huo unatarajiwa kuwa na mapambano ya utangulizi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment