Bondia Mada Maugo |
BONDIA nyota wa ngumi za kulipwa nchini, Mada Maugo anatarajiwa kupanda ulingoni mjini Arusha kuzichapa na Mustapha Katende kutoka Uganda katika pambano la kuwania ubingwa wa Mabara wa WBF.
Pambano hilo la uzani wa Super Middle la raundi 12 litafanyika Oktoba 28 kwenye ukumbi wa Triple A, jijini humo na kusindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi pamoja na burudani ya muziki wa kizazi kipya.
Akizungumza na MICHARAZO leo asubuhi, Maugo alisema awali pambano hilo litakalosimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania, PST, lilikuwa limkutanishe na bondia toka Iran, Gavad Zohrenvard.
Maugo alisema hata hivyo bondia huyo wa Iran amepatwa na dharura na hivyo kupangiwa Mganda ili kuonyeshana nae kazi siku ya pambano hilo.
"Natarajia kupanda ulingoni Oktoba 28 kwenye ukumbi wa Triple A mjini Arusha kuzichapa na Mganda, Mustapha Katende, ambapo pia tutasindikizwa na michezo mbalimbali ya utangulizi," alisema.
Alitaja baadhi ya mabondia watakaowasindikiza siku hiyo ni Robert Mrosso wa Arusha atakayepigana na Selemani Said 'Tall' wa Dar na Abbas Ally wa Arusha dhidi ya Joseph Marwa wa Zanzibar.
Bondia huyo aliyepanda mara ya mwisho ulingoni April mwaka huu kuwania ubingwa wa IBF-Mabara dhidi ya Francis Cheka na kupigwa, alisema amejiandaa vya kutosha kuweza kunyakua taji hilo la WBF dhidi ya Mganda.
"Naendelea kujifua kwa ajili ya kuhakikisha natwaa taji hilo, sambamba na kusaidia kutoa hamasa kwa vijana wenye vipaji vya ngumi mkoani Arusha," alisema Maugo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment