Vincent Barnabas (kushoto) akiwa dimbani na timu ya taifa , Taifa Stars |
WINGA machachari wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Vincent Barnabas amesema matokeo ya mechi za awali za Ligi Kuu Tanzania Bara zimeonyesha jinsi gani msimu huu utakuwa na ligi ngumu isiyotabirika kirahisi.
Aidha nyota huyo aliyewahi kutamba na timu za Kagera Sugar, Yanga na African Lyon, ameitabiria klabu yake ya Mtibwa Sugar kufanya vema tofauti na msimu uliopita ilipomaliza ikiwa nafasi ya nne.
Akizungumza na MICHARAZO, Barnabas, alisema kwa mechi za raundi tatu zilizokwisha kucheza mpaka sasa inaonyesha wazi ligi ya msimu huu sio nyepesi kama watu walivyokuwa wakiifikiria.
Nyota huyo alisema kutokana na mwenendo wa ligi hiyo, ni vigumu kutabiri mapema nani anayeweza kuwa bingwa kwa vile ligi bado haijatulia.
"Sio siri msimu huu ligi imeanza kuonyesha ni ngumu kwa aina ya matokeo yaliyopatikana, naamini ugumu huu umetokana na klabu zote kujipanga vema na kusaidia kuongeza ushindani," alisema.
Juu ya Mtibwa ambayo ilianza kwa sare dhidi ya Polisi Moro kabla ya kuilaza Yanga mabao 3-0 na kuzimwa na Azam mwishoni mwa wiki kwa bao 1-0, winga huyo alisema anaamini itafanya vema msimu huu tofauti na ligi iliyopita.
"Kwa namna tulivyo, naamini tutafanya vema, licha ya ugumu unaoonekana kwenye ligi ya msimu huu, wachezaji tumejipanga kuipigania timu ili imalize msimu tukiwa katika nafasi bora zaidi ya msimu uliopita," alisema Barnabas.
Kwa matokeo ya mwishoni mwa wiki, Mtibwa imejikuta ikiachwa nafasi ya sita ya msimamo ikiwa na pointi nne sawa na ndugu zao za Kagera Sugar na Yanga iliyozinduka kwa kuilaza JKT Ruvu mabao 4-1, ikizizidi uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment