MUIMBAJI anayekuja juu nchini wa bendi ya Vijana Jazz, Komweta Maneti 'Chiriku Mtoto', amefyatua wimbo mpya wa miondoko ya Bongofleva uitwao 'Doli Samwela'.
Katika wimbo huo msanii huyo ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa muziki wa dansi nchini, marehemu Hemed Maneti 'Chiriku', ameimba kwa kushirikiana na msanii aitwaye J-Sseni.
Wimbo huo ambao umeanza kusikika hewani umerekodiwa katika studio za C 9 na Komweta amesema kuwa ni kati ya nyimbo saba anazorekodi kwa ajili ya albamu yake binafsi nje ya bendi anayofanyia kazi ya Vijana Jazz.
Mwanadada huyo amewaomba mashabiki wa muziki nchini kuunga mkono ikizingatiwa hiyo ni kazi yake ya kwanza katika ulimwengu wa muziki.
"Naomba mashabiki wanisapoti kupitia wimbo huu na nyingine ambazo ninazitengeneza kabla ya kuitoa hadharani albamu yangu," alisema.
Hemed Maneti alikuwa mmoja wa magwiji wa muziki wa dansi nchini aliyedumu na bendi ya Vijana Jazz na kujijengea jina kubwa kabla ya kukumbwa na mauti miaka 25 iliyopita.
Mwanamuziki huyo aliyekuwa mtunzi mahiri alifariki Mei 31, 1990 na ni Komweta anayeonekana kufuata nyayo za baba yake huyo katika fani ya muziki.
Usikilize hapa chini
No comments:
Post a Comment