BADO hakijaeleweka tu. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuwa straika wake matata, Alexis Sanchez ataukosa mchezo wa mzunguko wa tatu wa Kombe la FA dhidi ya Sunderland ikiwa kama tahadhari.
Nyota huyo wa kimataifa wa Chile amekuwa nje ya Uwanja kwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya kupata majeruhi ya misuli katika mchezo dhidi ya Norwich City, Novemba 29 mwaka jana.
Sanchez alikuwa akitegemewa kurejea uwanjani kabla ya Krismasi, lakini alichelewa kupona na Wenger hayuko tayari kumwahisha kutokana na kukabiliwa na mechi ngumu za za Ligi Kuu dhidi ya Liverpool na Stoke City wiki ijayo.
Akizungumza katika mtandao wa klabu hiyo, Kocha Wenger amesema taarifa mbaya aliyonayo wiki hii ni kukosekana kwa Sanchez ambaye pamoja na kupona, lakini ameamua kumpa muda zaidi kama tahadhari.
Wenger ameendelea kudai kuwa kiungo Mikel Arteta atakuwepo katika kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza toka Novemba 21 wakati Tomas Rosicky naye ataanza mazoezi rasmi wiki ijayo baada ya kupona majeruhi yaliyokuwa yakimsumbua.
Arsenal ndio wanaoongoza kwa sasa msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa na pointi 42, mbili zaidi na ilizonazo Manchester City wanaofuata nyuma yao.
No comments:
Post a Comment