WAKATI Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyopewa
jukumu la kusimamia uchaguzi wa Yanga ikiongeza muda wa uchukuaji na urudishwaji fomu za uchaguzi huo, uongozi wa mabingwa hao wa soka umeamua kuonyesha ubabe.
Uongozi huo umetangaza kutoutambua uchaguzi huo wa Juni 25 na badala yake kuutangaza wao ambao utafanyika Juni 11 na zoezi la uchukuaji fomu za uchaguzi huo utakaoshirikisha wanachama wote wakiwamo wa zamani na wale wenye kadi za Benki ya Posta.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Baraka Deusdedit, alitangaza maamuzi hayo leo kwa madai kuwa, TFF haiwezi kuusimamia uchaguzi wao kwa vile hawawajui wanachama halali wa klabu hiyo.
Baraka alisema kuwa, wanaweza kuwekewa mamluki na kuivuruga Yanga ambayo kwa siku za karibuni imekuwa na mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi kiasi cha kutinga hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni rekodi kwa klabu za Ukanda wa Afrika Mashariki na Tanzania kwa ujumla.
Uongozi huo umesema zoezi la kuchukua na kurudisha fomu litaanza kesho Juni 2-3 kabla ya kufanyiwa usaili na baadaye kuendelea na taratibu nyingine ikiwamo pingamizi na kisha kuwasilisha majina ya wagombea watakaopitishwa kabla ya kampeni kuanza Juni 8-10 na uchaguzi kufanyika Juni 11 kisha matokeo yake kutangazwa Juni 12.
Hata hivyo hayo yanaendana kinyume na Kamati ya Uchaguzi wa TFF inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Wakili Msomi Alloyce Komba
kutokana na mipango yake, imesogeza mbele mchakato wa kuchukua na
kurejesha fomu mpaka Jumatatu Juni 6, 2016 saa 10:00 jioni. Isipokuwa
Jumamosi na Jumapili ya Juni 4 na 5, 2016.
Mpaka jana wanachama tisa (9) walikuwa wamechukua na kurejesha fomu. Wanachama
hao ni Aaron Nyanda na Titus Osoro wanaowania nafasi ya Makamu
Mwenyekiti kwa mujibu wa katiba ya mwaka 2010 inayotambulika serikalini
hadi sasa.
Wengine ni Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu
Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Omari Said kutoka Zanzibar
ambao wanawania nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji. Uchaguzi wa
Yanga unatarajiwa kufanyika Juni 25, 2016.
Fomu zinapatikana katika ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu
ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Vilevile utaratibu unafanyika ili
fomu ziweze kupatikana katika tovuti ya shirikisho www.tff.or.tz
Fomu
zinapatikana kwa gharama ya Sh 200,000 kwa
nafasi ya mwenyekiti na
makamu mwenyekiti na Sh
100,000 kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa
kamati ya utendaji.
No comments:
Post a Comment