Amina Athuman enzi za uhai wake |
SIMANZI. Mwandishi wa habari wa michezo wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Amina Athuman amefariki dunia asubuhi ya leo Jumapili na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi.
Malinzi ametuma salamu hizo kwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani kutokana na kifo hicho cha Amina, aliyekuwa visiwani Zanzibar kuripoti michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika juzi Ijumaa.
Katika salamu hizo ambazo pia zimeenda kwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Pinto; Rais Malinzi ameelezea kushtushwa kwake kwa taarifa za kifo cha ghafla cha Amina.
“Niseme tu wazi kuwa tangu kuanza kwa michuano ya Mapinduzi, nimekuwa nikifuatilia taarifa mbalimbali zinazotolewa na wanahabari. Huwa pia sikosi magazeti ya Uhuru na Mzalendo na kuona byline (jina la mwandishi) ya Amina. Mpaka matokeo ya fainali zilizofanyika Januari 13, mwaka huu.
“Sasa asubuhi hii nimepata taarifa za kifo chake, ama kwa hakika zinasikitisha. Ni kifo cha ghafla, ninavyomfahamu binti huyo ni mchapakazi hodari na mfano uko wazi kwani katika hali ya ujauzito alikuwa hakosi kufuatilia habari,” amesema Rais Malinzi.
Kadhalika, Rais Malinzi ametuma salamu hizo za rambirambi kwa familia ya marehemu Amina, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.
“Binafsi naona ni kama askari aliyefia vitani. Naweza kumwita ni shujaa, lakini ndivyo hivyo tena, huwezi kupingana na mipango ya Mungu, nimepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa, naomba wenzangu pia muwe na subira wakati huu mgumu ambao tasnia na Kampuni ya Uhuru Publications imepoteza mwanahabari mahiri.
Taarifa zinasema Amina alifariki dunia leo Jumapili Januari 15, 2017 akiwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mnazimmoja, iliyoko Zanzibar mara baada ya kujifungua jana kwa mtoto ambaye pia alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Hadi mauti yanamkuta alikuwa Mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo pamoja na gazeti la Burudani linalochapisha mahsusi habari za michezo na sanaa kabla ya hapo aliwahi pia kufanya kazi kampuni na Business Times Limited. Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Amina Athuman Mahala Pema Peponi. Inna Lillah wa Innaa Ilaihi Rajaajiuun.
No comments:
Post a Comment