STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, November 28, 2013

Tasnia ya Habari yapata pigo; Dunia mzobora hatunaye, kusikwa mchana huu

Dunia Mzobora enzi za uhai wake
TASNIA ya Habari imeendelea kupata mapengo baada ya Mwandishi  Mwandamizi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Dunia Mzobora (49) kufariki dunia ghafla asubuhi ya jana wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa Muhimbili alipokimbizwa kutoka Hospitali ya Aga Khan.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana zinasema kuwa, Mzobora aliyekuwa Kaimu Msanifu Mkuu wa gazeti la Uhuru, aliyewahi pia kuwa Naibu Mhariri wa Makala wa Mzalendo alifariki saa 12 asubuhi baada ya kuumwa ghafla usiku wa kuamkia jana akiwa nyumbani kwake.
Inaelezwa kuwa, mara baada ya kumaliza kulisimamia gazeti la Uhuru toleo la jana (Jumatano), hali yake ilibadilika na kulazimisha ndugu zake kumkimbiza hospitali ya Aga Khan, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na kuwahishwa Muhimbili na wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake aliaga dunia.
Marehemu Mzobora, aliyezaliwa April 6, 1964 Mwandege mkoani Kigoma anatarajiwa kuzikwa mchana huu katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Binafsi niliwahi kufanya kazi na Mzobora enzi za uhai wake wakati nafanya kazi Uhuru/Mzalendo na alikuwa ni mchapakazi, mcheshi na mwanamichezo.
Licha ya ucheshi, lakini marehemu Mzobora alikuwa makini katika kazi yake na alikuwa mmoja wa 'mabosi' wangu waliokuwa wakipenda kwa kujiweka watanashati karibu muda wote kiasi kilikuwa napenda kumuita 'Papaa'.
Mungu aiweke mahali pema roho ya marehemu Dunia Mzobora, yeye katangulia nasi tu nyuma yake na MICHARAZO inaungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu kwa kuwataka wawe na subira.

Super Nyamwela kutoka na Dully Sykes

KIONGOZI wa safu ya unenguaji wa bendi ya Extra Bongo, Hassan Mussa 'Super Nyamwela' amesema  yupo mbioni kupakua wimbo mpya atakaoimba na nyota wa muziki wa kizazi kipya, Prince Dully Sykes.
Akizungumza na MICHARAZO, Nyamwela alisema wimbo ambao hapendi kuutaja jina kwa sasa utarekodiwa katika studio za msanii huyo, ziitwazo Dhahabu Records za jijini Dar es Salaam.
Nyamwela alisema huo ni wimbo wa nne kuelekea kupakua albamu yake ya tatu baada ya awali kutoa 'Tumechete', 'Maneno' na kibao kinachoendelea kutamba kwa sasa wa 'Duvele Duvele'.
"Nipo katika maandalizi ya kuingia studio kurekodi wimbo wangu mwingine mpya ambao nitaimba na Dully Sykes, nao utakuwa kama Duvele kwa namna ya midundo yake, lengo kuwapa burudani mashabiki wangu," alisema Nyamwela.
Nyamwela alisema, anahofia kutaja jina la wimbo huo kwa sasa kwa madai ni mapema mno, pia akihofia kuibiwa 'idea' kutokana na kuwepo kwa mtindo wa baadhi ya wasanii kuiba kazi za wenzao na kuzitanguliza mapema hewani.
"Ningeutaja kwa sasa, lakini nahofia wasanii vilaza ambao hawaumizi vichwa kutoa kazi zao badala yake usubiri wasikie mawazo ya wenzao na kuwahi kutoa hewani," alisema.
Nyamwela aliyeanzia kwenye muziki wa disko kabla ya kuibngia kwenye makundi ya muziki wa dansi miaka ya 1990, aliwahi kutamba na albamu mbili za 'Master of the Tample na 'Afrika Kilomondo' alizoimba na wasanii wenye majina mkubwa nchini kama Ally Choki, Richard Maalifa na Sir Juma Nature.

Vigogo' vyaua' Ulaya, Madrid, Bayern, Man U, Juve kufuru tupu!

Watetezi, Bayern Munich wakishanmgilia mabao yao
MANCHESTER City imeifumua mabao 4-2 Viktoria Plzen Uwanja wa Etihad usiku huu katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mabao ya City yamefungwa na Aguero kwa penalti dakika ya 33, Nasri dkika ya 65, Negredo dakika ya 79 na Dzeko dakika ya 90, wakati mabao ya Viktoria Plzen yamefungwa na Horava dakika ya 43 na Tecl dakika ya 69.
MABINGWA watetezi, Bayern Munich wameendeleza wimbi lao la ushindi katika Ligi ya Mabingwa baada usiku wa kuamkia leo kuinyuka CSKA Moscow kwa mabao 3-1, huku Real Madrid ikiishindilia Galatasaray ya Uturiki mabao 4-1 na timu za Manchester zote zikipata ushindi mnono katika mechi zao.
Manchester United ikiwa ugenini nchini Ujerumani iliisasambua Bayer Leverkusen kwa mabao 5-0, huku wapinzani wao, Manchester City ikiwa nyumbani ikiicharaza Victoria Plzen kwa mabao 4-2.
Watetezi Bayern Munich waliipata ushindi wao wa 10 mfululizo na kupiku rekodi iliyowahi kuwekwa na Barcelona mwaka 2002 kwa mabao ya Arjen Robben, Mario Gotze na Thomas Muller aliyefungwa kwa penati.
Wakali wa Hispania, Real Madrid ikishuka dimbani bila nyota wake, Cristiano Ronaldo ilipata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Galatasaray licha ya kucheza pungufu baada ya Sergio Ramos akitolewa mapema kipindi cha kwanza kwa kadi nyukundu.
Winga, Gareth Bale aliwaongoza wenzake kupata ushindi huo uwanjawa nyumbani baada ya kutangulia kufunga bao la kwanza kabla ya Arbeloa kuongeza la pili katika dk ya 51, Di Maria dk ya 63 na Isco kuhitimisha karamu ya mabao dakika ya 80. Bao pekee la Waturuki lilifungwa dakika moja baada ya Bale kutangulia kuifungia Madrid, kupitia kwa Bulut.
Katika mechi nyingine Machi nyingine, Juventus ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Fc Copenhagen, huku Shakhtar Donetsk ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Real Sociedad na PSG ya Ufaransa ikipata ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Olympiacos ya Ugiriki jijini Paris.
Matokeo ya mechi zote zilizochezwa jana ni kama ifuatavyo;
Kundi A
Bayer Leverksuen 0-5 Manchester United
Shakhtar Donetsk 4-0 Real Sociedad
Kundi B
Real Madrid 4-1 Galatasaray
Juventus 3-1 FC Copenhagen
Kundi C
PSG 2-1 Olympiacos
Anderlecht 2-3 Benfica
Kundi D
Manchester City 4-2 Viktoria Plzen
CSKA Moscow 1-3 Bayern Munich