STRIKA
USILIKOSE
Sunday, August 12, 2012
Timu za Maafande wa JKT waandaliwa michuano maalum wazialika Coastal, Lyon
TIMU za soka za Coastal Union ya Tanga na African Lyon ya Dar es Salaam zinatarajiwa kushiriki michuano maalum ya 6 Bora zinazozihusisha timu za maafande wa JKT, kwa ajili ya kuziandaa vema na ushiriki wao wa Ligi Kuu.
Michuano hiyo itakayokuwa ikifanyika kila mwaka kulingana na uwepo wa timu hizo za maafande inatarajiwa kuanza siku ya Jumatano na itakuwa ikichezwa kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Msemaji wa michuano hiyo itakayochezwa kama ligi hadi kupata mshindi wake, Masau Bwire aliiambia MICHARAZO mapema leo kuwa timu nne za maafande wa JKT ndizo walengwa wakuu wa michuano hiyo ila katika kuipa msisimko zaidi wamezialika Coastal Union na African Lyon.
Bwire alisema wamezialika timu hizo kwa imani itazipa changamoto timu zao ili kuanza kuhimili mikikimikiki kabla ya kuanza kwa ligi kuu.
"Katika kuziandaa timu zetu za JKT na kuhakikisha zinafanya vema kwenye Ligi Kuu msimu huu, tumeziandalia michuano maalum ya Sita Bora ambayo itaanza Agosti 15 na tumezialika Coastal Union na African Lyon, kutokana na kuonekana zina viwango bora," alisema Bwire.
Alizitaja timu za JKT zilizolengwa kwa michuano hiyo ni wenyeji JKT Ruvu, Ruvu Shooting Stars, JKT Oljoro ya Arusha na JKT Mgambo Shooting ya Tanga iliyopanda daraja msimu huu.
Bwire alisema ratiba michuano hiyo itaanza kwa kuzikutanisha timu za JKT Ruvu na Ruvu Shooting siku ya Jumatano, siku inayofuata itakuwa zamu za JKT Oljoro dhidi ya Mgambo Shooting na Agosti 17 Coastal Union itavaana na Lyon.
"Hizo ni mechi za awali na ratiba kamili inatarajiwa kutolewa kuanzia Jumanne ili kuwapa fursa mashabiki wa soka kuifuatilia na hatimaye kujua nani atakayeibuka mshindi wa michuano hiyo maalum," alisema.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment