TFF YATOA ITC NNE, VODACOM, KLABU ZAMALIZANA LIGI KUU
SHIRIKISHO
la Soka Tanzania (TFF) limetoa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa
wachezaji wanne waliokuwa wakichezea timu mbalimbali nchini.
Ofisa Habari
wa TFF, Boniface Wambura alisema jana jijini kuwa, wachezaji
hao ni Tony Ndolo aliyejiunga na KCC ya Uganda kutoka Toto Africans, Felix
Amech Stanley aliyekwenda Bahla ya Oman kutoka Coastal Union, Ernest Boakye
kutoka Yanga aliyejiunga na Tripoli Athletics Club ya Lebanon na Derrick
Walulya aliyerejea URA ya Uganda kutoka Simba.
Katika hatua
nyingine, Wambura amesema wanamichezo 15 wamechukua fomu kuwania nafasi
mbalimbali za uongozi kwenye Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania
(TWFA) utakaofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao.
Aliwataja waliochukua
fomu za kuwania uenyekiti ni Lina Kessy, Isabellah Kapera na Joan Minja. Nafasi
ya Makamu Mwenyekiti imeombwa na Roseleen Kisiwa pekee wakati Katibu Mkuu ni
Amina Karuma na Cecilia Makafu. Macky Mhango pia ni mwombaji pekee aliyeomba
nafasi ya Katibu Msaidizi.
Alisema waombaji
watatu wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ni Furaha Francis, Juliet Mndeme na Zena Chande. Nafasi ya
Mhazini nayo ina mwombaji mmoja tu ambaye ni Rose Msamila.
Alisema Sophia
Charles, Rahim Maguza, Telephonia Temba na Jasmin Badar Soud wao wanaomba
nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho kwenye uchaguzi huo ambao
utaendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini ya Ombeni Zavalla.
Wakati huo
huo: Klabu za Ligi Kuu na mdhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya
Vodacom zimekutana jana mjini Dar es Salaam.
Wambura amesema
mazungumzo yalilenga kipengele ya upekee (exclusivity) kilichopo kwenye mkataba
wa udhamini ambacho kitaendelea kuwepo. Klabu zilikuwa zimeomba kwa mdhamini
kuangalia uwezekano wa kukiondoa.
Alisema pande
hizo zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja kwa ajili ya kuitafutia kila klabu
mdhamini binafsi kwa lengo la kuhakikisha zinashiriki kikamilifu katika ligi
hiyo na kwamba klabu zote zimeshapata vifaa kutoka kwa Vodacom ukiondoa African
Lyon ambayo ilitarajia kuchukua vifaa hivyo leo kutoka kwa mdhamini wa ligi
hiyo.
Kuhusu mchakato
wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Soka Tanzania (TAFCA), Wambura
alisema unaanza rasmi Septemba 30 mwaka huu kwa uchukuaji fomu kwa wagombea.
Alisema kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, fomu
kwa waombaji uongozi zitaanza kutolewa Septemba 30 mwaka huu, na mwisho wa
kuchukua na kurudisha fomu hizo ni Oktoba 4 mwaka huu.
Alisema fomu
hizo zinapatikana ofisi za TAFCA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar
es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 alasiri. Ada ya fomu kwa waombaji
wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi ni
sh. 200,000.
Alisema nafasi
zilizobaki za Mweka Hazina, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Wajumbe wa Kamati
ya Utendaji, ada ya fomu ni sh. 100,000. Uchaguzi wa TAFCA umepangwa kufanyika
Novemba 10 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment