STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, September 29, 2012

Barnabas asisitiza soka ya vijana

Vincent Barnabas (kulia) katika pambano la Taifa Stars na Msumbiji

WINGA wa timu ya Mtibwa Sugar ya ligi kuu ya Bara, Vincent Barnabas, amesema ili nchi irejeshe makali yake katika soka la kimataifa ni lazima shirikisho la mchezo huo, TFF, na wadau kuwekeza nguvu zao katika maendeleo ya vijana.
Barnabas, alisema mataifa yanayotamba kwenye soka duniani yaliwekeza fedha katika soka la vijana baada ya kuwa na mipango endelevu katika mchezo huo kuanzia ngazi za chini.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum na MJICHARAZO, Barnabas aliyewahi kuwika na timu za Kagera Sugar na Yanga, alisema timu za Tanzania kuanzia za taifa hadi klabu zinafanya vibaya katika michuano ya kimataifa kwa kupuuza soka la vijana.
"Mbali na kupuuza soka la vijana, pia maandalizi duni na kutokuwepo kwa mipango endelevu ya kuinua kandanda katika ngazi zote imekuwa ikiikwaza Tanzania kutamba kimataifa," alisema.
"Lazima tubadilike iwapo tunataka kufika walipo wenzetu."
Alisema nchi imejaliwa vijana wenye vipaji vya soka lakini vinaishia njiani kwa kutoendelezwa, hivyo ni lazima kuwepo na uwekezaji wa kutosha katika soka la vijana ili kuifanya nchi ing'are kama mataifa mengine.
Akizungumzia ligi kuu ya Bara iliyoingia katika mzunguko wa nne sasa alisema, "ni ngumu na haitabiriki.
"Ila kwa aina ya wachezaji tuliopo Mtibwa nadhani msimu huu utakuwa wetu licha ya upinzani toka kwa timu nyingine shiriki."
Mtibwa Sugar iliyomaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya nne, keshokutwa itacheza na Ruvu Shooting ikiwa na kumbukumbu ya kunyukwa bao 1-0 na Azam siku chache baada ya kuisasambua Yanga 3-0 mjini Morogoro.

No comments:

Post a Comment