TIMU ya soka ya Azam Fc, usiku wa kuamkia leo imefanikiwa kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara nyingine, baada ya kuilaza timu ngumu ya JKT Ruvu 3-0 katika mechi iliyocheza jijini Dar es Salaam.
Azam imeiengua Simba ambayo ndiyo iliyokuwa ikiongoza na leo inatarajiwa nao kushuka dimbani jioni kuumana na Prisons ya Mbeya, baada ya kufikisha jumla ya pointi 10 moja zaidi ya ilizonazo Simba.
Ushindi huo wa pili mfululizo kwa Azam ulipatikana katika mechi kali iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa na na kurushwa 'live' na kituo cha Super Sport kwa mabao yaliyofungwa na nyota wa timu hiyo, John Bocco 'Adebayor' na mapacha toka Ivory Coast, Kipre Tchetche na Kipre Balou.
Kipigo hicho cha jana ni cha tatu mfululizo kwa JKT Ruvu inayonolewa na kocha Charles Kilinda baada ya awali kunyukwa mabao 4-1 na Yanga kabla ya kulazwa mabao 2-1 na Simba katika mechi yao iliyopita.Katika muendelezo wa Tanzania Soccer Weekend leo jioni mabingwa watetezi Simba watakuwa wakijaribu kurejea kileleni kwa kuikaribisha Prisons ya Mbeya kabla ya kesho watani zao Yanga kuumana na African Lyon na Jumatatu kuwa zamu ya Mtibwa Sugar kupaishwa na Super Sport kwa kuumana na Ruvu Shooting.
Mechi ya mwisho katika mlolongo huo, ni pambano la watani wa jadi Simba na Yanga zinazotarajiwa kuvaana katika mechi yao ya kwanza kwa msimu huu ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa siku ya Jumatano.
Mechi hiyo ya watani inayosubiriwa kwa hamu kubwa inatarajiwa kurushwa hewani kuanzia majira ya saa 1;30 usiku siku hiyo ya Oktoba 3.
No comments:
Post a Comment