STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 27, 2012

Golden Bush: Klabu ya 'mastaa' wa soka iliyopania makubwa nchini * Yajipanga kuuza wachezaji wao barani Afrika kwanza kabla ya Ulaya


Nembo ya klabu ya Golden Bush






Kocha wa Golden Bush, Shija Katina akiwaelekeza wachezaji wake katika mazoezi ya timu hiyo

Kikosi kamili cha Golden Bush (wa kwanza kulia) ni kocha Shija Katina



KIU kubwa ya kutaka kuinua na kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana pamoja na kutoa ajira kwa vijana hao kupitia soka ndiko kulikofanya baadhi ya nyota wa zamani wa soka nchini kuungana na kuanzisha timu yao ya Golden Bush.
Nyota hao wa zamani wakiongozwa na Ally Mayay, Wazir Mahadhi 'Mandieta' , Abuu Ntiro, Said Swedi 'Panucci', Salum Swedi 'Kussi', chini ya makocha Shija Katina na Madaraka Selemani waliungana na kuiasisi timu hiyo mpya.
Wakiwa wamepeana majukumu ndani ya timu hiyo iliyo chini ya muasisi na

mlezi wao, Onesmo Wazir 'Ticotico', kiu yao kubwa ni kuifanya klabu hiyo kuwa ya mfano nchini kutokana na malengo na mikakati waliyoijiwekea.
Moja ya malengo ya timu hiyo inayojiandaa na ushiriki wa Ligi ya TFF wilaya ya Kinondoni ni kuendeleza vipaji na kuwawezesha vijana wenye uwezo wa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi wakitimiza ndoto zao.
Uongozi wa timu hiyo yenye maskani yake Sinza, Dar es Salaam japo iliasisiwa

Mabibo, ulisema haitakimbilia kuwapeleka wachezaji wao kucheza soka Ulaya badala yake wataanzia kuwapeleka nchi za barani Afrika kwanza.
Meneja wa timu, Wazir Mahadhi alisema wanaamini kucheza soka la kulipwa

barani Afrika ni njia nzuri ya kuwapa nafasi wachezaji wao kupata uzoefu wa kuhimili mikikimikiki kabla ya kusonga mbele kwenye ushindani zaidi kisoka.
Mahadhi alisema ndiyo maana katika timu yao wamejumuisha wachezaji wa umri wa miaka 17-23 tu, kwa kuamini umri huo ni sahihi kwa wachezaji kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa.
Naye mlezi wa klabu hiyo, Onesmo Wazir 'Ticotico' alisema tayari wameanza mipango ya kujenga uhusiano na klabu kadhaa za barani Afrika ili kurahisisha mipango yao wakianzia na nchi ya Msumbiji.
"Tayari tumeshaanza kutekeleza mikakati yetu, tunatarajia kupeleka wachezaji wetu nchini Msumbiji, tunatarajia miezi sita ijayo tutapanua wigo zaidi katika mahusiano na klabu nyingine za nje," alisema Ticotico.
Ticotico, 'membaz' wa zamani wa Friends of Simba na mjumbe wa zamani wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Simba chini ya uongozi wa akina ismail Rage,

alisema wamepanga miaka miwili ijayo Golden Bush iwe mbali kimaendeleo.
"Tumelenga kuja kuanzisha 'academy' ya soka itakayohusisha vijana wenye umri kati ya miaka 14-17,  pia tuweze kuwalipa wachezaji wetu mishahara tofauti na posho tunazowapa kwa sasa," alisema.

KWA NINI?
Ticotico alisema saababu kuu ya kuasisiwa kwa timu hiyo ilitokana na yeye na wachezaji hao nyota wa zamani kukerwa kuona vipaji vya soka vya vijana vikipotea mitaani bila kutumiwa wala kunufaisha taifa na wachezaji wenyewe.
Japo alikiri wanatambua changamoto kubwa zilizopo mbele yao ili kuifikisha

Golden Bush mahali walikokusudia, bado anaamini timu yao itafika mbali kutokana na walivyojipanga hasa  kuifanya timu yao iwe yenye ushindani.
Ticotico, Mahadhi na kocha Shija Katina walisema kwa nyakati tofauti wakati ilipoanzishwa klabu hiyo ilikuwa kwa ajili ya kushiriki mabonanza, lakini kule kuona vijana wengi wakijitokeza kucheza pamoja nao iliwapa wazo la kuiboresha.
Walisema ilipoanzishwa timu hiyo ilikuwa na wachezaji wasiozidi 20, ila kwa sasa wamesajiliwa 28 kwa ajili ya Ligi ya TFF inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

MATARAJIO
Mbali na kuifanya iwe klabu ya mfano, Mahadhi alidai wanataka kuipandisha timu hiyo daraja sambamba na kutoa ajira kwa vijana kama alivyofafanua mlezi wao juu ya mipango ya kuanzisha 'chuo' na kuuza wachezaji nje ya nchi.
Hata hivyo, Mahadhi wenzake walisema kitu cha muhimu wanachoomba ni kupata sapoti kwa wadau wa soka nchini wakiwamo wafadhili kujitokeza kuwapiga tafu ili kutimiza malengo yao.
"Hatuwezi kufanikiwa kama hatutaungwa mkono na wadau kuanzia watu binafsi hadi makampuni kwa ajili ya udhamini," alisema.
Aliongeza kuwepo kwa wadhamini wa kutosha na sapoti toka kwa wadau wa

soka kutaiwezesha Golden Bush kutimiza ndoto za kuwa klabu ya mfano sawia na kuwapa faraja wachezaji wanaotegemea vipaji vya kuwanufaisha.

NIDHAMU
Katika moja ya vitu ambavyo uongozi na benchi la ufundi la timu hiyo inavyoviangalia ni suala la nidhamu ndani na nje ya uwanja.
Makocha, Shija Katina na Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio', walisema suala la nidhamu ndicho kipaumbele cha kuchukuliwa kwa vijana kuichezea timu hiyo na suala hilo linaendelea kuzingatiwa hata sasa timu ikiwa inazidi kuimarika.
Katina, alisema bahati nzuri wachezaji walionao ni waelewa na wenye malengo ya kweli ya kufika mbali kisoka na hivyo wanazingatia nidhamu na kujituma kwa moyo bila kusukumwa.
Alisema nidhamu hiyo ya wachezaji na ushirikiano uliopo baina yao na uongozi mzima wa Golden Bush ndiyo iliyowawezesha katika mechi 15 walizokwishacheza moja sasa kushinda mara saba ikiwamo kuzilaza Mtibwa Sugar, 94 KJ na kuisimamisha Kagera Sugar waliotoka nao sare miongoni mwa sare mbili walizopata.
"Tumecheza mechi 15 tuimeshinda saba na kupoteza sita na sare mbili baadhi ya timu tulizocheza nazo ni za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza, na tuliweza kuzisimamisha kwa vile wachezaji wana nidhamu ndani na nje ya dimba hata kwa mechi za kirafiki."

SAFU YAKE
Klabu hiyo ya Golden Bush iliyoasisiwa April mwaka jana kabla ya kupata usajili kamili mwishoni mwa mwaka jana, ina safu kamili ya uongozi ambapo Mwenyekiti wake ni Ally Mayay akisaidiwa na Salum Swedi.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo ni Majaliwa Mwaigaga akisaidiwa na Henry Morris, huku Meneja akiwa ni Wazir Mahadhi, na makocha wake ni Shija Katina na Madaraka Seleman.
Mlezi wa timu hiyo ambayo imekuwa ikifanya mazoezi yake kwenye uwanja wa Kinesi Ubungo na wakati mwingine Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni Onesmo Wazir na ikipata sapoti kubwa na nyota wa zamani akina Abuu Ntiro, Yahya Issa, Said Swedi, Shaaban Kisiga na waasisi wengine baadhi wakiendelea kucheza soka ngazi ya ligi kuu na daraja la kwanza.
Add caption

No comments:

Post a Comment