MASHINDANO ya ngumi za ridhaa ya klabu bingwa ya taifa yaliyopangwa
kuanza kufanyika jana Novemba 26 hadi Novemba -30 mwaka huu yamesogezwa mbele hadi Januari 29 hadi
Februari 3 mwakani.
Katiku Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa nchini (BFT), Makore
Mashaga alisema juzi kuwa, wamelazimika kusogeza mbele mashindano hayo
hadi mwakani kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na timu shiriki kushindwa
kukamilisha taratibu, ikiwa ni pamoja na kutothibitisha ushiriki wake
katika tarehe iliyopangwa.
Kwa mujibu wa Mashaga, sababu zingine ni timu shiriki kushindwa
kuwasilisha majina na picha za mabondia wake pamoja na kulipa ada ya
ushiriki ya sh. 200,000.
"Hadi leo hakuna hata timu moja iliyokamilisha utaratibu huo kwa nia ya
kupanga mashindano vizuri ili yawe na hadhi ya taifa kwa kuzingatia
sheria za Chama cha Ngumi za Ridhaa cha Dunia (AIBA)," alisema.
"Sababu kama hizi mara nyingi zimesababisha mashindano mengi kuendeshwa
kwa kiwango cha chini na lawama nyingi kuelekezwa kwa BFT bila ya
kufahamu sababu za msingi," aliongeza.
Mashaga alisema pia kuwa, kozi ya waamuzi iliyopangwa kuanza Novemba
11-30 mwaka huu ilishindwa kufanyika kutokana na washiriki kushindwa
kukamilisha taratibu za ushiriki ikiwa ni pamoja na kulipa ada kwa
wakati.
Kutokana na BFT kuwa na majukumu mengine, Mashaga alisema kozi hiyo sasa
imepangwa kufanyika Januari 15 hadi Februari 4 mwakani na mazoezi ya
vitendo yatafanyika wakati wa mashindano ya klabu bingwa.
Mashaga alisema kwa sasa, BFT imeweka nguvu kubwa katika usajili wa
makocha, waamuzi, mabondia na madaktari ili waweze kutambulika kwa ajili
ya kujiunga na mashirikisho ya ngumi za kulipwa.
No comments:
Post a Comment