STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 25, 2013

Mbio za kinyang'anyiro cha Redd's Miss Tanzania zaanza rasmi


Mshindi wa Redd's Miss Tanzania 2012, Brigitte Alfred

HARAKATI za awali za kumsaka Redd’s Miss Tanzania zinaanza rasmi mwishoni mwa wiki hii wakati kutakapokuwa na kinyang’anyiro cha kuwapata warembo wa vitongoji katika maeneo mbalimbali nchini wakiwamo wa vyuo vya elimu ya juu (Redd’s Miss High Learning), imefahamika.
Taarifa kutoka kwa waandaaji wa shindano la Redd’s Miss High Learning mkoani   Morogoro, zinaeleza kuwa mwakilishi wao atasakwa mkoani humo kesho. Imefahamika vilevile kuwa Jumamosi, pia kutakuwa na kinyang'anyiro cha aina hiyo mkoani Dodoma wakati atakaposakwa mrembo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), mwakilishi wa vyuo vya elimu ya juu kutoka mikoa ya Kagera na Mwanza.
Mratibu wa shindano la Redd’s Miss Morogoro High Learning, Verdian Kamugisha, alisema kuwa kila kitu kimekamilika na kutakuwa na burudani za kutosha wakati watakapokuwa wakimsaka mwakilishi wao.
“Tumekamilisha kila kitu na warembo wote wako katika hali nzuri na kutakuwa na burudani za kutosha. Wakazi wa Morogoro waje kuwaunga mkono warembo wetu ili hatimaye tupate mwakilishi atakayepeperusha vyema bendera ya mkoa huu," alisema Kamugisha.
Mratibu wa Shindano la Redd’s Miss UDOM, Rachel Matina, alisema vilevile kuwa wamekamilisha maandalizi wanaamini kwamba kazi iliyobaki ni kwa watu wa Dodoma kujitokeza keshokutwa kushuhudia namna washiriki kutoka Chuo Kikuu Dodoma walivyopania kulitwaa taji la Redd’s Miss Tanzania mwaka huu.
Joseph Rwebangira anayeratibu shindano la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wa mikoa ya Kagera na Mwanza, alisema mrembo wao atapatikana keshokutwa katika shindano litakalofanyika jijini Mwanza na wanachosubiri sasa ni kwa mashabiki wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi ili kuwaunga mkono warembo wao na pia kupata burudani mbalimbali.
Katika hatua nyingine, shindano la kumsaka mrembo wa kitongoji cha Hai mkoani Kilimanjaro linatarajiwa pia kufanyika mjini humo mwishoni mwa wiki hii, kama ilivyo kwa kinyang'anyiro cha kuwasaka warembo wa kitongoji cha Tarime mkoani Mara.
Hivi sasa, shindano la Redd’s Miss Tanzania hudhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original. Mshindi wa shindano hilo ngazi ya taifa huiwakilisha nchi katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia.

No comments:

Post a Comment